Friday, October 26, 2012

Hutba ya mwisho ya Mtume!!

Swali:
Assalaam aleykum,Mimi ni mwislamu na naomba mnijuje hutba ya mwisho ya Mtume (S.A.W).

Jibu:
Kila nikiisoma khutba hii huhisi kama imetolewa jana wakati ni karne kumi na nne na thuluthi (miaka 1427) tayari zimepita. Kila nikiisoma khutba hii huyatafakari tena maneno haya machache ya Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) lakini yamejaa mafundisho na kusheheni hazina ya elimu na mausio . Khutba iliyokusudiwa waislamu wote duniani popote walipo, kizazi baada ya kizazi ,karne baada ya karne. Ni wosia ambao ametuagiza Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) tuufikishe kwa kila muislamu.

Khutba hii ilitolewa na Mtume Muhammad (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) tarehe 09 Dhul Hijja mwaka wa 10 Hijriya kwenye Mlima Arafah huko Makkah – Saudi Arabia - alipokwenda Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) kufanya ibada ya Hijja ambayo pia ilijulikana kama Hijja ya kuaga. Baada ya kumshukuru Allah (Subhaanahu Wata’ala) na kumsifu, Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) alianza khutba kwa kusema:
---
“ Enyi watu! Nisikilizeni maneno yangu vizuri , kwani sidhani kama baada ya mwaka huu nitakuwa pamoja nanyi. Hivyo sikilizeni kwa makini nitakayoyasema na (maneno haya ) mfikishieni kila asiekuwepo hapa leo.”

“Enyi watu! Hakika damu zenu na mali zenu ni takatifu kwenu kama mlivyoufanya mwezi huu kuwa mtakatifu na mji huu kuwa mtukufu .
”Rudisheni amana mlizokabidhiwa kwa wenyewe wanaostahiki . Msimdhuru yeyote ili nanyi msije mkadhuriwa . Kumbukeni mtakuja kukutana na mola wenu naye atahesabu amali zenu. Allah (Subhaanahu Wata’ala) amekukatazeni kula riba . Hivyo riba zote zimeondoshwa na mna haki ya kubaki na rasilmali (mitaji) yenu . Hamna haki ya kudhulumu wala kudhulumiwa . Allah (Subhaanahu Wata’ala) ameharamisha riba na riba zote za Abbaas ibn Abdul Muttallib zimeondoshwa ”

Kila haki ya kisasi iliyekuwepo enzi za Ujahiliya imefutwa na haki ya kwanza kuifuta ni ya Rabiah ibn Harith ibn Abdul Muttalib “

“Enyi watu! washirikina wanajaribu kuakhirisha (kuchelewesha) kalenda ili wafanye kuwa Salla Allahu ‘Alayhi Wasallama idadi ya ile (miezi) aliyo itukuza Allah na kulifanya halali jambo ambalo Allah(Subhaanahu Wata’ala) ameliharamisha na kulikataza jambo ambalo Allah(Subhaanahu Wata’ala) ameliruhusu . Miezi kwa Allah(Subhaanahu Wata’ala) ni kumi na miwili . Mine kati yao ni mitakatifu, mitatu ikiambatana (Dhul Qaadah, Dhul Hijjah na Muharram) na mmoja (Rajab) uko kati ya Jumada (ya mwanzo na ya mwisho) na Shaaban.
“Jiepusheni na shetani kwa ajili ya kuilinda dini yenu . Tayari (shetani ) amekata tamaa kwamba ataweza kuabudiwa katika ardhi hii milele lakini bado ana mikakati ya kukupotezeni hivyo tahadharini nae katika mambo mengine .”

“Enyi watu ! ni kweli mna haki juu ya wanawake na wao pia wana haki juu yenu . Kumbukeni mmewachukua kuwafanya wake zenu kwa amana ya Allah(Subhaanahu Wata’ala) na mmehalalishiwa (kustarehe) nao kwa neno lake” . “Nnakuusieni kuwatendea wema wanawake na kuwa na huruma kwao kwani ni wake zenu na wasaidizi wenu .Ni haki yenu kuhakikisha hawafanyi urafiki na msiyemuafiki na ni juu yao kutokufanya jambo la uchafu lililo wazi na pindipo wakifanya Allah amewapa idhini ya kuwahama kwenye malazi na kuwapiga kipigo kisichoumiza. Ikiwa watatekeleza majukumu yao basi na wao watakuwa na haki ya kulishwa na kuvishwa kwa wema.”
“ Enyi watu, nisikilizeni kwa utulivu , mcheni Allah(Subhaanahu Wata’ala) , msali sala tano kila siku, fungeni katika mfungo wa Ramadhan na toeni Zakah. Tekelezeni ibada ya Hijjah ikiwa mna uwezo.”

“ Binadamu wote wametokana na Adam na Hawaa , hakuna mbora kati ya mwarabu na asiyekuwa mwarabu , wala asiekuwa mwarabu kwa mwarabu , wala mweupe kwa mweusi au mweusi kwa mweupe isipokuwa kwa Taqwa( kumcha Allah).
“Eleweni kila muislamu ni ndugu kwa muislamu na waislamu wote ni ndugu. Hatohalalishiwa muislamu kitu chochote isipokuwa kila alichopewa kwa ridhaa na ndugu yake . Wala msidhulumu nafsi zenu . Na msisahau kwamba kuna siku mtakutana na mola wenu na mtahesabiwa amali zenu. Hivyo tahadharini msije mkapotea baada yangu”
“Enyi watu ! Hakuna tena Mtume baada yangu na hakuna dini nyengine itakayokuja. Ninakuachieni vitu viwili ambavyo mkishikamana navyo hamtopotea milele navyo ni QURAAN na SUNNA (mwenendo) zangu.”
“Wale wote walionisikiliza waufikishe ujumbe huu kwa wengine, na wengine waufikishe kwa watakaofuatia na inawezekana hawa wa mwisho wakayafahamu vyema maneno yangu kuliko hawa walionisikiliza moja kwa moja.”

“Ewe mola shuhudia kwamba nimefikisha ujumbe kwa watu wako”

Ndugu zangu waislamu, hazina kama hizi ndizo tulizoagizwa kufikishiana. Inshaallah kila atakaepata ujumbe huu ahakikishe anamfikishia mwengine kama tulivyoagizwa na Al Habib Mustafa (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) na asaa inawezekana miongoni mwetu kuwapata tutakaomsikiliza Mtume(Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) na kumfahamu vyema na hivyo kuufuata mwenendo wake . Tumuombe Allah(Subhaanahu Wata’ala) atujaalie miongoni mwao. Amin

Saturday, October 6, 2012

Jina la Tanzania lilitungwa na mwislamu?

Swali:
Hello, mimi naitwa Getruda naishi zanzibar.
Swali langu ni "eti ni kweli jina la Tanzania liliundwa na mwislamu?"

JIBU:
Ni kweli kabisa.Anaitwa Mohammed Iqbal na kwa sasa anaishi uingereza.

Huyu bwana aliyebuni jina la Tanzania ni Muhindi na Dini yake ni AHMADIYA MUSLIM JAMAAT TANZANIA majina yake ni MOHAMMED IQBAL DAR.
Mohammed alizaliwa Mkoani Tanga miaka ya 1944, Baba mzazi wa Mohammed alikuwa Daktari huko mkoani Morogoro alikuwa anaitwa Dkt. T. A. DAR  alikuwa Tanganyika kuanzia mwaka 1930.

Mohammed Iqbal Dar alipata elimu yake ya Msingi Mkoani Morogoro shule ya Msingi H H D AGHAKHAN kwa sasa ni Shule ya Serikali na baada ya hapo alikuja baadae kujiunga na Chuo cha Mzumbe akasoma Kidato cha Kwanza mpaka cha Sita.


Mohammed anasema alikuwa Maktaba akijisoma gazeti la Tanganyika Standard, siku hizi Daily News, akaona Tangazo linasema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar unafahamika kama Republic of Tanganyika and Zanzibar jina likaonekana refu sana kwa hiyo Wananchi wote wakaombwa Washiriki kwenye shindano la Kupendekeza jina moja litakalo zitaja nchi zote mbili yaani Tang
anyika na Zanzibar Mohammed Iqbal Dar anasema aliamua kuingia kwenye Shindano na hivi ndivyo alianza Safari ya Kubuni Jina la Muungano.

Kwanza anasema alichukua karatasi akaandika Bismillah Raahman Rahimu hii ni kutokana na Imani yake na baada ya hapo akaandika jina la Tanganyika baada ya hapo akaandika Zanzibar halafu akaandika jina lake Iqbal halafu akaandika jina la Jumuiya yake ya Ahmadiya baada ya Hapo akamrudia tena Mwenyezi Mungu akamwomba amsaidie ili apate jina zuri kutoka katika majina hayo aliyokuwa ameyaandika. Baada ya hapo Mohammed Iqbal Dar alichukua herufi tatu kutoka Tanganyika yaani TAN na kwa upande wa Zanzibar akachukua Herufi tatu za Mwanzo ZAN ukiunganisha unapataTANZAN alivyoona hivyo akachukua I herufi ya kwanza katika jina lake la Iqbal na akachukuaA kutoka jina la dini yake yaani Ahmadiyya kwa maana hiyo ukiongeza herufi hizi mbili I na Akwenye TANZAN unapata jina kamili TANZANIA akalisoma jina akaliona ni zuri lakini akajiridhisha pia kwamba akiongeza herufi hizo za I na A kwenye TANZAN italeta maana kwakuwa nchi nyingi za Afrika zinaishia na IA, mfano EthiopIA, ZambIA, NigerIA, TunisIA, SomalIA, GambIA, NamibIA, LiberIA, MauritanIA alivyoona hivyo akaamua apendekeze kuwa jina TANZANIA ndio litumike kuwakilisha nnchi hizi mbili yaani Tanganyika na Zanzibar kwa maana hiyo jina TANZANIA limezaliwa kutoka majina manne majina hayo ni Tanganyika, Zanzibar, Iqbal na Ahmadiyya.

Mohammed Iqbal Dar baada ya kupata jina hilo akalituma jina hilo kwenye kamati ya kuratibu Shindano. Baada ya Muda mwingi kupita baba yake na Mohammed Iqbal Dar alipokea barua nzito kutoka Serikalini ikiwa inasomeka kama ifuatavyo…

REPRESENTED BY THE
MINISTRY OF INFORMATION AND TOURISM, TANZANIA
TO
MOHAMED IQBAL DAR
IN RECOGNATION OF THE ACHIEVEMENT OF CHOOSING THE NEW NAME FOR THE
UNITED REPUBLIC OF TANGANYIKA AND ZANZIBAR NAMELY
“REPUBLIC OF TANZANIA”
DURING THE NATIONAL COMPETITION DAY IN 19TH NOVEMBER 1964
I A WAKAL
MINISTER FOR INFORMATION AND TOURISM

Barua hiyo pia ilisema...

“Utakumbuka kuwa miezi michache iliyopita ulituandikia kutupa ushauri kuhusu jina jipya la Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na wewe pamoja na wananchi wenzio 16 ulishauri nnchi yetu iitwe Tanzania. Nafurahi kukuarifu kuwa mshirikiane ile Zawadi ya sh. 200 iliyoahidiwa na leo nakuletea check ya sh. 12/50 ikiwa ni hisa yako katika zile sh.200. Nashukuru sana kwa jitihada ya kufikiri jina la Jamuhuri yetu.”

Barua ikasainiwa na Idrisa Abdul Wakil aliyekuwa Waziri wa Habari na utalii wakati huo.

Sasa kwa nini Mohamedi Iqbal Dar anadai yeye kuwa mshindi pekee wakati barua ilikuwa inaonyesha kulikuwa na washindi wengine 15 ambao nao walishinda?

Jibu ni kuwa wakati wa kutolewa kwa zawadi hizo hakuna aliyejitokeza zaidi ya Bwana Mohammed Iqbal Dar na Bwana Yusufal Pir Mohamed ambaye hata hivyo alikosa sifa baada ya kushindwa kutoa barua ya kumpongeza kuwa ameshinda kwa madai kuwa Barua ameipoteza, hivyo Wizara ya Habari na Utalii iliamua kumtangaza Mohammed Iqbal Dar kuwa Mshindi na kumpatia zawadi yote ya sh.200/; pamoja na Ngao.

Bwana Mohammedi Iqbal Dar anasema anachosikitika ni kuwa mchango wake bado Watanzania hawathamini mchango wake lakini yeye anaipenda Tanzania na anajivunia kuwa Mtanzania japo anadhani dini yake ya Uislamu ndiyo tatizo hawataki kutambua mchango wake ila anaamini kuwa siku moja ukweli utajulikana.

Hayo ni maelezo ya Mohammed Iqbal ambaye kwa sasa anaishi Uingereza kwa kuwa huko ndiko alipata kazi eneo la Birmigham b35 6ps UK, Dar– es-Salaam House, 18 TURNHOUSE 
ROAD, PHONE 44 121-747-9822


Animated Social Gadget - Blogger And Wordpress Tips Twitter Bird Gadget