Wednesday, November 14, 2012

Yesu alibatizwa? Na Je, Biblia Imeruhusu Ala Za Muziki Na Misalaba Kanisani

SWALI:
Je ni kweli Yesu Alibatizwa? Na Je, Biblia Imeruhusu Ala Za Muziki Na Misalaba Kanisani?


JIBU:Shukrani zetu za dhati kwa swali lako zuri japokuwa kufanya hivyo sio kuwa una dhamana ya uhakika kuweza kuwavuta Wakristo katika Uislamu. Biblia yenyewe tuelewe ina utata mkubwa katika mas-ala mengi hivyo kwa Mkristo aliyebobea huweza kukuvuruga wewe bila wasiwasi. Pia tufahamu hakuna kitabu kilichoteremshwa na Mwenyezi Mungu kinachoitwa Biblia.
Mas-ala mengi yana utata katika Biblia hivyo kuwachanganya hata wenye kuifuata Dini hiyo. Tukija katika suala lako twaweza kusema yafuatayo:
Ama kuhusu ubatizo wa Yesu Biblia inatueleza wazi kuwa alibatizwakama mistari ifuatayo inavyosema:
  1. "Mara tu Yesu alipobatizwa" (Mathayo 3: 16). Aliyembatiza ni Yohane kama ilivyo katika msitari wa 15 katika kitabu hicho cha Mathayo.
  2. "Yohane mbatizaji alitokea jangwani…Siku hizo, Yesu alitoka kutoka Nazareti, mji wa Galilaya, akabatizwa na Yohane katika mto Yordani" (Marko 1: 4 – 9).
  3. "Watu wote walipokuwa wamekwisha batizwa, Yesu naye alibatizwa" (Luka 3: 21).
  4. Kitabu cha Yohane kinatueleza kuwa Yohane alikuwa anabatiza lakini hakumbatiza Yesu, kwani alishuhudia tu kuwa Yesu ni mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi ya ulimwengu (Yohane 1: 24 – 29).
Ama kuhusu vinanda na magitaa (ala za muziki) yapo mistari yanayoruhusu na mengine kukataza. Hilo linatuweka sisi katika hali ya utata kuwa ni lipi lililo sawa. Hebu tutazame baadhi ya maandiko:
  1. "Mwenyezi-Mungu asema hivi: 'Nazichukia na kudharau sikukuu zenu; siifurahii mikutano yenu ya kidini. Mjaponitolea sadaka zenu za kuteketezwa za nafaka, mimi sitakubali kuzipokea; na sadaka zenu za amani za wanono mimi sitaziangalia kabisa. Ondoeni mbele yangu kelele za nyimbo zenu! Sitaki kusikiliza muziki wa vinubi vyenu" (Amosi 5: 21 - 23). Tunaelezwa katika kitabu hicho hicho tena: "Nyinyi mnapenda kuimba ovyo na sauti ya vinubi na kubuni ala mpya za muziki mkimwiga mfalme Daudi" (Amosi 6: 5). Hizi ibara zinatuelezea nini sisi? Ibara ya awali inakataza muziki na ya pili inatuelezea kuwa kulikuwa kukibuniwa ala mpya za muziki kwa kumwiga mfalme Daudi. Je, ibara ya pili inaunga mkono muziki au inakataza? Kipengele kimoja kinakataza lakini cha pili kinaunga. Hili linatubabaisha zaidi kuhusu suala hili.
  2. Mistari ifuatayo inaruhusu suala hilo kwa uwazi kabisa. Hebu tutazame haya: "Mwimbieni kwa sauti Mungu, nguvu yetu mshangilieni Mungu wa Yakobo; vumisheni wimbo wa shangwe, pigeni ngoma, chezeni zeze na kinubi cha sauti nzuri. Pigeni tarumbeta kutangaza mwezi mwandamo, na pia mwezi mpevu, wakati wa sikukuu yetu" (Zaburi 81: 1 – 3). Hata hivyo, suala linakuja ni nani aliyeruhusu jambo hiloikiwa Zaburi 72: 20 inasema: "Mwisho wa sala za Daudi, mwana wa Yese". Ikiwa ibara hii ndio mwisho wa Zaburi ya Daudi, sasa hii sura ya 81 inayoruhusu nyimbo na ala za muziki imeruhusiwa na nani? Bila shaka, itakuwa imeruhusiwa na mwingine na wala sio Daudi.
  3. Katika Agano la Kale tunaelezwa: "Kwa nini ulitoroka kisiri, ukanihadaa wala hukuniarifu ili nipate kukuaga kwa shangwe, nyimbo, matari na vinubi" (Mwanzo 31: 27). Ibara hii haiwezi kuchukuliwa kama ni ruhusa kwani aliyesema ni mshirikina ambaye katika msitari wa 32 amesema: "Lakini kwa nini uliiba vinyago vya miungu yangu?"
  4. Ruhusa nyingine inapatikana katika Kutoka 15: 20: "Basi nabii Miriamu, dada yake Aroni, akachukua kigoma mkononi, na wanawake wengine wote wakamfuata wakiwa na vigoma vyao wakicheza". Hii ni taarifa ya furaha iliyopatikana kwa upande wa wanawake pale Firauni alipoangamizwa na Mwenyezi Mungu wakiwa wanawake wapo peke yao.
Suala hili mbali na kuwa na utata dalili ya ibara zenye nguvu ni zile zinazokataza matumizi ya ala hizo.
Ama utumiaji wa msalaba katika kuvaa umezagaa kabisa kwa Wakristo wa zamani na wa sasa. Kufanya hivyo kwao ni kukumbuka kule kusulubiwa kwa Yesu kwa ajili ya dhambi za wanadamu nao waingie katika kusamehewa dhambi zao hapa duniani na kurithi uzima wa milele Siku ya Qiyaama. Hata hivyo, tukisoma katika Biblia tunapata kuwa Yesu hakusulubiwa kwani aliyesulubiwa atakuwa amelaaniwa. Hebu tutazame mistari ifuatayo:
  1. "Kama mtu amefanya kosa la jinai linalompasa auawe na akauawa kwa kutundikwa mtini" (Kumbukumbu la Sheria 21: 23).
  2. "Kristo alitukomboa kutoka katika laana ya sheria kwa kujitwalia laana hiyo kwa ajili yetu; maana Maandiko yanasema: 'Yeyote aliyetundikwa msalabani amelaaniwa" (Wagalatia 3: 13).
Hakika ni kuwa wenye kuamini kuwa Yesu kasulubiwa na misalaba kwa ajili ya kusamehewa dhambi wanapingana na Biblia. Hebu tusome mistari ifuatayo:
  1. "Maana ninachotaka kwenu ni upendo na si dhabihu, kumjua Mungu na si kutoa sadaka za kuteketezwa" (Hosea 6: 6).
  2. "Basi, kajifunzeni maana ya maneno haya: 'Nataka huruma, wala si dhabihu'. Sikuja kuwaita watu wema, bali wenye dhambi" (Mathayo 9: 13).
  3. "Kama tu mngejua maana ya maneno haya: 'Nataka huruma wala si dhabihu', hamngewahukumu watu wasio na hatia" (Mathayo 12: 7).
Kwa hivyo Yesu hakuja kuwa dhabihu, yaani kuuliwa msalabani bali amekuja kuwaokoa wenye hatia waingie katika mafundisho ya haki na hivyo kupata msamaha wa Mwenyezi Mungu.

Yesu ni Alfa na Omega?

SWALI:
Mbona nyie waislamu mnakataa kwama Yesu si Mungu wakati yeye anasema kuwa ni Alfa na Omega?

JIBU:
Ni kweli kuwa katika Kitabu cha Ufunuo 1, ayah ya 8, inaonyeshwa kuwa Yesu alisema yafuatayo kuhusu yeye mwenyewe: “Mimi ni Alfa na Omega”, asema Bwana, aliyeko, aliyekuwako na anayekuja, Mwenye Nguvu”. Hizi ni sifa za Mwenyezi Mungu. Hivyo, Yesu, kulinagana na Wakristo wa mwanzo, hapa anadai uungu. 

Hata hivyo, hayo ni mojawapo ya maandiko yaliyo na makosa ya kiuchapishaji katika biblia za King James Version KJV.
-Katika 
RSV, wanazuoni wa Biblia walisahihisha tafsiri na kuandika: “Mimi ni Alfa na Omega”, asema Bwana Mungu, aliyeko, aliyekuwako na anayekuja, Mwenye Nguvu”. 


-Masahihisho pia yalifanywa kwa New American Bible (Biblia Mpya ya Marekani) iliyochapishwa na Katoliki. Tafsiri ya Ayah hiyo imerekebishwa ili kuiweka katika muktadha wa sawa kaa ifuatavyo: “Bwana Mungu anasema: ‘Mimi ni Alfa na Omega, yule aliyeko na aliyekuwako na anayekuja, Mwenye Nguvu’”. 
Kwa masahihisho haya, ni dhahiri kuwa hii ni kauli ya Mwenyezi Mungu wala sio kauli ya Nabii ‘Iisa (YESU).

Waislamu Wanaamini Nini Kuhusu Yesu?

SWALI:
NATAKA KUJUA KUWA WAISLAMU MNAAMINI NINI HASA KUHUSU YESU?

JIBU:
Waislamu wanamheshimu na kumtukuzasana Yesu (‘Alayhis Salaam). wanamchukulia kuwa ni mmojawapo kati ya Mitume wakuu wa Mwenyezi Mungu kwa watu. Qur-aan inathibitisha kuzaliwa kwake na Bikira Maryam, na ipo Surah ya Qur-aan yenye jinaMaryam. Qur-aan inaeleza kuzaliwa kwa Yesu kama ifuatavyo: “Na pale Malaika waliposema: Ewe Maryam! Hakika Mwenyezi Mungu Anakubashiria (mwana)kwa neno litokalo kwake. Jina lake ni Masihi ‘Iysa mwana wa Maryam, mwenye hishima katika dunia na Akhera, na miongoni mwa waliokaribishwa (kwa Mwenyezi Mungu). Naye atazungumza na watu katika utoto wake na katika utuuzima wake, na atakuwa katika watu wema. Maryam akasema: Mola wangu Mlezi! Vipi nitampata mwana na hali hajanigusa mwanaadamu? Mwenyezi Mungu Akasema: Ndivyo vivyo hivyo, Mwenyezi Mungu Huumba Apendacho. Anapohukumu jambo, huliambia: Kuwa! Likawa.” Qur-aan, 3:45-47)
Yesu alizaliwa kimiujiza kwa amri ya Mwenyezi Mungu ambayo ilimleta Aadam kuwa kiumbe pasina baba. Mwenyezi Mungu Amesema:
 Hakika mfano wa ‘Iysa kwa Mwenyezi Mungu ni kama mfano wa Aadam; Alimuumba kwa udongo kisha Akamwambia: Kuwa! Basi akawa.” (Qur-aan, 3:59)
Wakati wa mpango wake wa kiutume, Yesu alifanya miujiza mingi. 
Mwenyezi Mungu Anatuambia kuwa Yesu alisema: “Mimi nimekujieni na Ishara kutoka kwa Mola Mlezi wenu, ya kwamba nakuundieni kwa udongo kama sura ya ndege. Kisha nampuliza anakuwa ndege kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na ninawaponesha vipofu wa tangu kuzaliwa na wakoma, na ninawafufua maiti kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, na ninakwambieni mnacho kila na mnacho weka akiba katika nyumba zenu.” (Qur-aan, 3:49)
Waislamu wanaamini kwamba Yesu hakusulubiwa. Mpango wa maadui wa Yesu ulikuwa ni kumsulubu, lakini Mwenyezi Mungu Alimwokoa na Akamnyanyua Kwake. Mfano wa Yesu ukawekwa kwa mtu mwingine. Maadui wa Yesu walimchukua mtu huyu na wakamsulubu kwa kudhani alikuwa Yesu. Mwenyezi Mungu Amesema: “...Walisema: Sisi tumemuua Masihi ‘Iysa, mwana wa Maryam, Mtume wa Mwenyezi Mungu - nao hawakumuuwa wala hawakumsulubu, bali walifananishiwa tu...” Qur-aan, 4:157)
Si Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wala Yesu aliyekuja kubadili mafundisho ya msingi ya Dini ya kumwamini Mungu Mmoja, yaliyoletwa na Mitume waliotangulia, bali ni kuyathibitisha na kuyajadidisha.

Waislamu huamini pia kwamba Mwenyezi Mungu aliteremsha kitabu kitukufu kwa Yesu kiitwacho Injiyl, ambacho huenda sehemu yake ingalimo ndani ya Agano Jipya katika mafundisho ya Mwenyezi Mungu kwa Yesu. Hata hivyo, hii haimaanishi kuwa Waislamu wanaiamini Biblia tuliyo nayo katika zama hizi kwa sababu si maandiko ya asili yaliyoteremshwa na Mwenyezi Mungu. Yamefikwa na mabadiliko, nyongeza na uondoshaji. Haya yalisemwa pia na Kamati iliyokuwa na majukumu ya kuipitia (na kuisahihisha na kuleta bora zaidi) The Holy Bible (Revised Standard Version). Kamati hii iliundwa na wasomi thelathini na wawili waliokuwa wajumbe wa Kamati hiyo. Walidhamini upitiaji na ushauri wa Bodi ya Ushauri yenye wawakilishi khamsini wa madhehebu shirikishi. Kamati ilisema katika Dibaji ya The Holy Bible (Revised StandardVersion), uk. iv: “Wakati mwingine kuna ushahidi dhahiri kuwa kitabu hiki kimepatwa na taabu ya upitishaji, lakini hakuna tafsiri yoyote kati ya hizo inayotoa utunzaji wa asili wa kutosheleza. Tunachoweza hapa ni kufuata tu, maoni yaliyo bora ya wasomi kama njia ya kufikia katika linayoelekea kuwa ndilo tengenezo jipya la andiko la asili.” Kamati hiyo ilisema tena katika dibaji, uk. Vii: “Nukuu zimeongezwa ambazo zinaonesha mabadiliko, nyongeza au uachaji wa msingi ndani ya mamlaka za kale (Mt 9.34; Mk 3.16, 7.4; LK 24.32, 52 n.k.).” Kuhusu maelezo zaidi juu ya mabadiliko ya Biblia, tafadhali tembelea www.islam-guide.com/bible]
                                                                                                                                  
The Aqsa Mosque in Jerusalem
(Tafadhali, tembelea www.islam-guide.com/pillars kwa ajili ya maelezo zaidi juu Yesu katika Uislamu.)

Krismasi ina Ushahidi wa Biblia?

SWALI:
Mimi ni mkristo nimekuwa nikiwauliza viongozi wangu wa kiriho lakini sipati jibu lenye hoja, na wengine huniambia kuwa katika dini yetu kuna "DOGMA" mengine hayaulizwi, ila mimi nahitaji kujua ukweli ili niwe huru.

Swali langu ni hili" Je, Krismasi ina ushahidi wa kibiblia? na je ni kweli Yesu alizaliwa 25 Desemba? Santa Claus (Baba Krismas) ni nani? Je Yesu na wanafunzi wake walishawahi kusheherekea Krismasi? Pia kama mtanipa historia ya krismasi ntafarijika sana.


JIBU:
Asante sana, lifuatalo ni jibu la maswali yako:
Historia ya Krismasi
Wakati wa zama za kale, siku ya mwisho ya majira ya baridi huko sehemu za Kusini kulisherehekewa mfano wa usiku ambao mungu wa Mama Watakatifu alijifungua mtoto akijulikana kuwa ni mungu wa Jua. Pia (siku hii) inaitwa Yule, siku ambayo inasherehekewa mno kwa kurushwa pashpashi. Ambapo kila mtu atacheza na kuimba ili kuliamsha jua kutokana na usingizi wake mnono wa majira ya baridi.
Wakati wa Warumi, iliadhimishwa kwa kumsifu Satunusi (mungu wa mavuno) na Mithrasi (mungu wa kale wa nuru), huo ni mtindo wa kuabudia jua ambao umekuja ukitokea Syria hadi Urumi. Karne kabla ya madhehebu ya Sol Invictus, ilitangaza ya kwamba, majira hayo ya baridi sio ya milele, na kwamba maisha yanasonga mbele, na ni mualiko wa kubaki kwenye nguvu nzuri.
Siku ya mwisho ya majira ya baridi huko sehemu za mviringo za Kusini ni baina ya siku ya 20 au 22 Disemba. Warumi waliadhimisha Saturnalia baina ya tarehe 17 na 24 Disemba.
Wakristo wa kale
Ili kuepuka kuchunguzwa wakati wa sherehe ambazo ni za wapagani, Wakristo wa kale walikaa majumbani mwao pamoja na mtakatifu Saturnalia. Kwa vile idadi ya Wakristo iliongezeka na mila zao zikaenea, sherehe zikachukua shuruti za Kikristo. Lakini, Makanisa ya kale hakika hayakusherehekea mwezi wa Disemba kwa kuzaliwa Kristo hadi alipokuja Telesforusi Telesphorus, ambaye alikuwa askofu wa pili wa Roma kutoka mwaka 125 hadi 136 AD, askofu huyo ndiye aliyetangaza kwamba huduma za Kanisa zifanywe wakati huu ili kuadhimisha “Kuzaliwa kwa Bwana wetu na Mwokozi”. Hata hivyo, kwa vile hakuna mtu hata mmoja aliye na uhakika wa mwezi ambao amezaliwa Kristo, kawaida ya Uzawa ulikumbukwa Septemba, ambao ulikuwa ni wakati wa Sherehe za Kiyahudi za Trumpetsi (kwa sasa ni Rosh Hashanah). Ukweli ni kuwa, kwa zaidi ya miaka 300, watu walielewa kuzaliwa kwa Yesu katika tarehe tofauti.
Katika mwaka 274 AD, kikomo cha jua kiliangukia tarehe 25 Disemba. Mfalme wa Roma aitwaye Aurelian alitangaza tarehe hiyo kama ni “Natalis Solis Invicti”, ‘Sherehe Ya Kuzaliwa Jua Lisiloshindikana’. Katika mwaka 320 AD, Papa Julius I aliitangaza tarehe 25 Disemba kama ni tarehe rasmi ya kuzaliwa Yesu Kristo.
Mnamo mwaka 325 AD, Krismasi ilitangazwa rasmi, lakini kiujumla haikutiliwa maanani. Mtakatifu Constantine, ambaye ni Mfalme wa mwanzo wa dhehebu la Ukristo la Kirumi, aliitanguliza Krismasi kama ni sherehe isiohamishika kwa tarehe 25 Disemba. Pia aliitanguliza Jumapili kama ni siku kuu ndani ya siku saba za wiki, na aliitanguliza (Pasaka) kama ni sherehe yenye kuhamishika. Mnamo mwaka 354 AD, Askofu Liberius wa Rumi, alitoa amri rasmi kwa wafuasi wake kusherehekea kuzaliwa kwa Yesu ndani ya tarehe 25 Disemba.
Hata hivyo, ingawa Constantine aliifanya rasmi tarehe 25 Disemba kama ni sherehe ya kuzaliwa Kristo, Wakristo wakiitambua kama ni tarehe ya sherehe iliyofanana na mapagani, hawakushiriki katika mambo mazuri (kwa siku hii) iliyopangwa na Askofu. Krismasi ilishindwa kupata utambulisho wa kilimwengu miongoni mwa Wakristo hadi kipindi cha hivi karibuni. Huko Uingereza England, Oliver Cromwell alizipiga marufuku sherehe za Krismasi baina ya miaka 1649 na 1660 kupitia kwa inayoitwa Sheria za Rangi Samawati Blue Laws, akiamini kwamba iwe ni siku ya kumuabudu mungu tu.
Hamu ya kuifurahia sherehe ya Krismasi ilikirimiwa pale Waprotestanto (Wakristo wasiokubali baadhi ya mafundisho ya Kanisa la Kirumi) walipokimbia uchunguzi kwa kutorokea sehemu za makoloni yote duniani. Hata hivyo, Krismasi bado haikuwa ni sikukuu halali hadi miaka ya 1800. Na, weka akilini, hakukuwa na picha ya Baba Krismasi (Santa Claus) kwa wakati huo.
Krismasi inaanza kuwa maarufu
Umaarufu wa Krismasi ulianza ghafla mnamo mwaka 1820 kutokana na kitabu cha Washington Irving The Keeping of Christmas at Bracebridge Hall ‘Kuiadhimisha Krismasi Kwenye Jukwaa La Bracebridge’. Mnamo mwaka 1834, Malkia wa Uingereza aitwaye Victoria, alimkaribisha mumewe wa Kijerumani Prince Albert ndani ya Ngome ya Windso Windsor Castle, akimuonesha tamaduni za mti wa Krismasi Christmas tree na Nyimbo Za Kumsifu Yesu Kristocarols ambazo ziliadhimishwa Uingereza kwa Mfalme wa Uingereza. Mwaka 1834, wiki moja kabla ya Krismasi, Charles Dickens alichapisha Nyimbo za Kumsifu Yesu za Krismasi Christmas Carols(ambapo aliandika kwamba Scrooge alimuamrisha Cratchit kufanya kazi, na kwamba Baraza Kuu la Marekani US Congress lilikutana Siku ya Krismasi). Ilikuja kuwa ni maarufu mno hadi kufikia kwamba sio makanisa wala serikali kukana umuhimu wa sherehe za Krismasi. Mnamo mwaka 1836, Alabama ilikuja kuwa ni taifa la mwanzo ndani ya Marekani kutangaza Krismasi kama sikukuu halali. Mnamo mwaka 1860, mfananishi illustrator wa Marekani aitwaye Thomas Nast alichukua kutoka hadithi za Kiingereza kuhusu Mtakatifu Nicholas, muangalizi mtakatifu wa watoto, kumtengeneza Baba Krismasi Father Christmas. Mwaka 1907, Oklahoma ilikuwa ni ya mwisho miongoni mwa mataifa ya Marekani kutangaza Krismasi kama ni sikukuu halali. Mwaka baada ya mwaka, nchi za dunia nzima zilianza kuitambua Krismasi kama ni siku ya kusherehekea kuzaliwa kwa Yesu.
Nakuombea Krismasi Njema Have a merry Christmas
Leo, mambo mengi yasiyokuwa ya Kikristo yananasibishwa ndani ya Krismasi. Yesu alizaliwa mwezi wa Machi, bado siku yake ya kuzaliwa inasherehekewa Disemba ya 25, wakati wa solstice. Sherehe za Krismasi zinamalizikia siku kumi na mbili za Krismasi (Disemba 25 hadi Januari 6), ni idadi hiyo hiyo ya siku ambazo zilisherehekewa na wapagani wa ki-Rumi wakale kwa kuadhimisha kurudi kwa jua. Hivyo, hakuna mshangano wowote kwamba Wakristo waliosafi puritans – au Wakristo wasiotaka mabadilikoconservative – watahamaki kwa Krismasi kuwa “sio ya kidini kama ilivyotakikana kuwa,” wakisahau kwamba Krismasi haikusherehekewa hata kidogo hadi siku za hivi karibuni.
Yesu Alisemaje Kuhusu Krismasi?
Mazoea ya Krismasi
Mti ulio bora wa Krismasi unanunuliwa. Ukipambwa kwa madoido yenye kung’ara pamoja na kumetameta, unasimamishwa karibu na dirisha. Maduka yanajazana wanunuzi wakisaka zawadi na vile viduchu vinasubiri kwa hamu kubwa ya Baba Krismasi Santa.
Ni mshughuliko na ni homa ya Krismasi Christmas fever, umewahi kufikiri kabla? Je, Biblia au Yesu aliwahipo kusababisha homa ya Krismasi?Tafakari juu ya mchanganuo ufuatao kuhusu Krismasi, na ukweli utakuja kuwa wazi zaidi na zaidi.
Je, Krismasi Ina Ushahidi wa Biblia?
Neno ‘Krismasi’ halipo ndani ya Biblia. Biblia ilifunga midomo ya sherehe yote inayohusiana na Krismasi, isipokuwa kwa kitu kimoja; upambaji wa mti. Biblia wenyewe inashutumu upambaji wa miti (ya Krismasi):
“Mila za watu si chochote, wanakata mti kutokana na msitu, na mchongaji anauchonga kwa patasi yake, wanaupamba kwa fedha na dhahabu, wanaugandanisha kwa nyundo na misumari ili usipate kutikisika” (Jeremia 10-3,4).
Wazungu wa ki-Pagani kabla ya Ukristo, waliamini miujiza kwamba miti ya kijani ina nguvu maalum za ulinzi. Hakika, matumizi ya Miti ya Krismasi imeanza hivi karibuni tu mwa karne ya 17 hukoStrasbourg, Ufaransa na kutoka huko ukaenea hadi Ujerumani, Uingereza na baadaye Marekani. “Ibada ya miti ilikuwa ni jambo la kawaida kwa dini miongoni mwa watu wa Tyutoniki Teutonic na Skandinavia Scandinavia wa Ulaya ya kaskazini kabla ya kuingia kwenye Ukristo…Walowezi wa ki-Jerumani walileta mila za Mti wa Krismasi kwenye makoloni ya Kimarekani mnamo karne ya 17. Kufikia karne ya 19, matumizi yake yalienea sehemu tofauti”. (Angalia Encyclopedia ya Compton, Toleo la 1998)
Je, Yesu Alizaliwa Disemba ya 25?Si tarehe ya Disemba 25 wala tarehe nyengine yoyote iliyotajwa ndani ya Biblia kuhusu kuzaliwa kwa Yesu. Ilikuwa ni hivyo hadi kufikia mwaka 530 C.E kwamba mtawa monk aitwaye Dionysus Exigus, aliweka tarehe isiyobadilika ya kuzaliwa kwa Yesu kuwa ni Disemba 25. “Kulingana na taratibu za ki-Roma, alikosea kuipanga tarehe ya kuzaliwa kwa Kristo (yaani, miaka 754 baada ya kupatikana nchi ya Rumi) kama ni Disemba 25, mwaka 753”. (Angalia: Encyclopedia Britannica, toleo la mwaka 1998) Tarehe hii ilichaguliwa ili iendane pamoja na sikukuu ambazo zimeshagandana na imani za kipagani.
Mapagani wa Kirumi walisherehekea Disemba 25 kama ni ya kuzaliwa kwa ‘mungu’ wao wa nuru, aitwaye Mithra.
“Mnamo karne ya pili A.D, hiyo sherehe ya Mithra ilikuwa ni ya kawaida zaidi ndani ya Ufalme wa Rumi kuliko Ukristo, ambayo ilizaa mifanano iliyo mingi” (The Concise Columbia Encyclopedia, toleo la mwaka 1995).
‘Waungu’ wengine wakipagani waliozaliwa Disemba ya 25 ni: Hercules mtoto wa Zeuz (Wagiriki); Bacchus, ‘mungu’ wa mvinyo (Warumi); Adonis, ‘mungu’ wa Kigiriki, na ‘mungu’ Freyr wa Ugiriki-mapagani wa Roma.
 Je, Vipi Kuhusu Baba Krismasi Santa Claus?
Kama viumbe visivyokuwa binaadamu aliens watafika duniani katika wakati wa Krismasi, bila ya shaka wataamini Krismasi kuwa ni sherehe ya kufurahikia kuzaliwa kwa Baba Krismasi Santa. Majina ya ‘Santa Claus’, hayamo popote ndani ya Biblia.
Hata hivyo, Mtakatifu Nikolas Saint Nicholas (Baba Krismasi Santa Claus) alikuwa ni mtu halisi, askofu, ambaye alizaliwa miaka 300 baada ya Yesu. Kwa mujibu wa hekaya za kale, alikuwa ni mtu mwenye huruma mno na alitenga nyakati za usiku kwenda kutoa zawadi kwa mafukara. Baada ya kifo chake mnamo Disemba ya 6, watoto wa shule huko Ulaya walianza kusherehekea siku hiyo kwa karamu kila mwaka.
Baadaye Malkia Victoria aliibadilisha sherehe hiyo kutoka Disemba ya 6 kuwa ni Disemba ya 24 kuamkia Krismasi.
Je, Yesu au Wafuasi Wake Waliwahi Kusherehekea Krismasi?Kama Yesu alimaanisha kwa wafuasi wake kusherehekea Krismasi, angeliifanyia kazi yeye mwenyewe na kujikusanya pamoja na wafuasi wake. Hakuna sehemu iliyotajwa ndani ya Biblia kwamba kuna mfuasi yeyote aliyewahi kusherehekea kuzaliwa kwa Yesu kama Wakristo wanavyofanya leo.
“Kanisa halikupatapo kuweka sikukuu kwa ajili ya sherehe za tukio la Krismasi hadi ilipofika karne ya 4” (Angalia: Encyclopedia ya Grolier)
Hivyo, tunaona kwamba sio Biblia wala Yesu na wafuasi wake waliosema kitu kuhusu sherehe za Krismasi ambazo sasa zinahusisha viingilio vya sherehe, biashara, na matumizi yaliyochupa mpaka, ni utovu wa akili kwa mfananisho wowote wa imani.

Tuesday, November 13, 2012

Naomba ushahidi wa utume wa YESU (A.S)..

SWALI:
Hello "Majibu Yetu",

Mimi ni mkristo lakini huwa nasikia mkisema kuwa Yesu ni mtume tuu na kuna rafiki yangu mwislamu alinionesha kwenye kitabu chenu katika 5:75 kuwa Yesu si chochote ila ni Mtume tuu, na wamekwishapita mitume kabla yake.

Swali langu ni hili"Naomba ushahihi wa  Biblia kuwa Yesu alitumwa."


JIBU:
Asante sana kwa swali lako.
Kwa kweli yapo maandiko mengi sana katika Biblia yanayothibitisha kuwa Yesu (Amani iwe naye) ni mtume tu.

Haya hapa chini baadhi tuu ya maandiko hayo:
YOHANA 5:24    
"Kweli nawaambieni, anayesikia neno langu, na kumwamini yule aliyenituma, anao uzima wa milele. Hatahukumiwa kamwe, bali amekwisha pita kutoka kifo na kuingia katika uzima.

YOHANA 5:30
     "Mimi siwezi kufanya kitu kwa uwezo wangu mwenyewe. Mimi nina hukumu kama ninavyosikia kutoka kwa Baba, nayo hukumu yangu ni ya haki. Nia yangu si kufanya nipendavyo mwenyewe, bali apendavyo yule aliyenituma.

 YOHANA 5:36
     Lakini mimi nina ushahidi juu yangu ambao ni mkuu zaidi kuliko ule wa Yohane. Kwa maana kazi ninazofanya, kazi alizonipa Baba nizifanye, ndizo zinazonishuhudia kwamba Baba ndiye aliyenituma.

 YOHANA 5:37
     Naye Baba aliyenituma hunishuhudia. Ninyi hamjapata kamwe kusikia sauti yake, wala kuuona uso wake.
       
YOHANA 7:16
     Hapo Yesu akawajibu, "Mafundisho ninayofundisha si yangu, bali ni yake yeye aliyenituma.

YOHANA 7:28
     Basi, Yesu alipokuwa anafundisha Hekaluni alipaaza sauti na kusema, "Ati mnanijua; hata nilikotoka mnakujua! Hata hivyo, sikuja kwa mamlaka yangu mwenyewe; ila yeye aliyenituma mimi ni wa kweli, nanyi hamumjui.

YOHANA 7:29
     Lakini mimi namjua kwa sababu nimetoka kwake, naye ndiye aliyenituma."

YOHANA 7:33
     Yesu akasema, "Bado niko nanyi kwa muda mfupi, kisha nitamwendea yule aliyenituma.
       
YOHANA 8:16
     Hata nikihukumu, hukumu yangu ni ya haki kwa sababu mimi siko peke yangu; Baba aliyenituma yuko pamoja nami.

YOHANA 8:18
     Mimi najishuhudia mwenyewe, naye Baba aliyenituma, ananishuhudia pia."

YOHANA 8:26
     Ninayo mengi ya kusema na kuhukumu juu yenu. Lakini yule aliyenituma ni kweli; nami nauambia ulimwengu mambo yale tu niliyoyasikia kutoka kwake."

YOHANA 8:29
     Yule aliyenituma yuko pamoja nami; yeye hakuniacha peke yangu kwani nafanya daima yale yanayompendeza."
       
YOHANA 6:38
     kwani nimeshuka kutoka mbinguni si kwa ajili ya kufanya matakwa yangu, ila kutimiza matakwa ya yule aliyenituma.

YOHANA 6:39
     Na matakwa ya yule aliyenituma ndiyo haya: nisimpoteze hata mmoja kati ya wale alionipa, ila niwafufue wote Siku ya mwisho.
       
YOHANA 12:44
    Kisha Yesu akasema kwa sauti kubwa, "Mtu aliyeniamini, haniamini mimi tu, ila anamwamini pia yule aliyenituma.

YOHANA 12:49
    Mimi sikunena kwa mamlaka yangu mwenyewe, ila Baba aliyenituma ndiye aliyeniamuru niseme nini na niongee nini.
       
MATAYO 10:40
   "Anayewakaribisha ninyi, ananikaribisha mimi; na anayenikaribisha mimi, anamkaribisha yule aliyenituma.
       
MARKO 9:37
       "Anayempokea mtoto kama huyu kwa jina langu, ananipokea mimi; na anayenipokea mimi, hanipokei mimi tu, bali anampokea yule aliyenituma."
       
LUKA 9:48
  akawaambia, "Mtu yeyote anayempokea mtoto huyu mdogo kwa jina langu, ananipokea mimi; na yeyote anayenipokea mimi, anampokea yule aliyenituma. Maana yule aliye mdogo kuliko wote kati yenu ndiye aliye mkubwa kuliko wote."
       
LUKA 10:16
        Halafu akasema, "Anayewasikiliza ninyi, ananisikiliza mimi; na anayekataa kuwapokea ninyi, anakataa kunipokea mimi. Yeyote anayekataa kunipokea, anakataa kumpokea yule aliyenituma."
       
YOHANA 4:34
     Yesu akawaambia, "Chakula changu ni kufanya anachotaka yule aliyenituma na kuitimiza kazi yake.
       
YOHANA 9:4
       Kukiwa bado mchana yatupasa kuendelea kufanya kazi za yule aliyenituma; maana usiku unakuja ambapo mtu hawezi kufanya kazi.
       
YOHANA 13:20
    Kweli nawaambieni anayempokea yule ninayemtuma anaponipokea mimi; na anayenipokea mimi, anampokea yule aliyenituma."
       
YOHANA 14:24
    Asiyenipenda hashiki maneno yangu. Na neno mlilosikia si langu, bali ni lake Baba aliyenituma.
       
YOHANA 15:21
    Lakini hayo yote watawatendeeni ninyi kwa sababu ya jina langu, kwani hawamjui yeye aliyenituma
.
       
YOHANA 16:5
     Lakini sasa namwendea yule aliyenituma; na hakuna hata mmoja wenu anayeniuliza: `Unakwenda wapi?`
Animated Social Gadget - Blogger And Wordpress Tips Twitter Bird Gadget