Friday, October 26, 2012

Hutba ya mwisho ya Mtume!!

Swali:
Assalaam aleykum,Mimi ni mwislamu na naomba mnijuje hutba ya mwisho ya Mtume (S.A.W).

Jibu:
Kila nikiisoma khutba hii huhisi kama imetolewa jana wakati ni karne kumi na nne na thuluthi (miaka 1427) tayari zimepita. Kila nikiisoma khutba hii huyatafakari tena maneno haya machache ya Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) lakini yamejaa mafundisho na kusheheni hazina ya elimu na mausio . Khutba iliyokusudiwa waislamu wote duniani popote walipo, kizazi baada ya kizazi ,karne baada ya karne. Ni wosia ambao ametuagiza Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) tuufikishe kwa kila muislamu.

Khutba hii ilitolewa na Mtume Muhammad (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) tarehe 09 Dhul Hijja mwaka wa 10 Hijriya kwenye Mlima Arafah huko Makkah – Saudi Arabia - alipokwenda Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) kufanya ibada ya Hijja ambayo pia ilijulikana kama Hijja ya kuaga. Baada ya kumshukuru Allah (Subhaanahu Wata’ala) na kumsifu, Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) alianza khutba kwa kusema:
---
“ Enyi watu! Nisikilizeni maneno yangu vizuri , kwani sidhani kama baada ya mwaka huu nitakuwa pamoja nanyi. Hivyo sikilizeni kwa makini nitakayoyasema na (maneno haya ) mfikishieni kila asiekuwepo hapa leo.”

“Enyi watu! Hakika damu zenu na mali zenu ni takatifu kwenu kama mlivyoufanya mwezi huu kuwa mtakatifu na mji huu kuwa mtukufu .
”Rudisheni amana mlizokabidhiwa kwa wenyewe wanaostahiki . Msimdhuru yeyote ili nanyi msije mkadhuriwa . Kumbukeni mtakuja kukutana na mola wenu naye atahesabu amali zenu. Allah (Subhaanahu Wata’ala) amekukatazeni kula riba . Hivyo riba zote zimeondoshwa na mna haki ya kubaki na rasilmali (mitaji) yenu . Hamna haki ya kudhulumu wala kudhulumiwa . Allah (Subhaanahu Wata’ala) ameharamisha riba na riba zote za Abbaas ibn Abdul Muttallib zimeondoshwa ”

Kila haki ya kisasi iliyekuwepo enzi za Ujahiliya imefutwa na haki ya kwanza kuifuta ni ya Rabiah ibn Harith ibn Abdul Muttalib “

“Enyi watu! washirikina wanajaribu kuakhirisha (kuchelewesha) kalenda ili wafanye kuwa Salla Allahu ‘Alayhi Wasallama idadi ya ile (miezi) aliyo itukuza Allah na kulifanya halali jambo ambalo Allah(Subhaanahu Wata’ala) ameliharamisha na kulikataza jambo ambalo Allah(Subhaanahu Wata’ala) ameliruhusu . Miezi kwa Allah(Subhaanahu Wata’ala) ni kumi na miwili . Mine kati yao ni mitakatifu, mitatu ikiambatana (Dhul Qaadah, Dhul Hijjah na Muharram) na mmoja (Rajab) uko kati ya Jumada (ya mwanzo na ya mwisho) na Shaaban.
“Jiepusheni na shetani kwa ajili ya kuilinda dini yenu . Tayari (shetani ) amekata tamaa kwamba ataweza kuabudiwa katika ardhi hii milele lakini bado ana mikakati ya kukupotezeni hivyo tahadharini nae katika mambo mengine .”

“Enyi watu ! ni kweli mna haki juu ya wanawake na wao pia wana haki juu yenu . Kumbukeni mmewachukua kuwafanya wake zenu kwa amana ya Allah(Subhaanahu Wata’ala) na mmehalalishiwa (kustarehe) nao kwa neno lake” . “Nnakuusieni kuwatendea wema wanawake na kuwa na huruma kwao kwani ni wake zenu na wasaidizi wenu .Ni haki yenu kuhakikisha hawafanyi urafiki na msiyemuafiki na ni juu yao kutokufanya jambo la uchafu lililo wazi na pindipo wakifanya Allah amewapa idhini ya kuwahama kwenye malazi na kuwapiga kipigo kisichoumiza. Ikiwa watatekeleza majukumu yao basi na wao watakuwa na haki ya kulishwa na kuvishwa kwa wema.”
“ Enyi watu, nisikilizeni kwa utulivu , mcheni Allah(Subhaanahu Wata’ala) , msali sala tano kila siku, fungeni katika mfungo wa Ramadhan na toeni Zakah. Tekelezeni ibada ya Hijjah ikiwa mna uwezo.”

“ Binadamu wote wametokana na Adam na Hawaa , hakuna mbora kati ya mwarabu na asiyekuwa mwarabu , wala asiekuwa mwarabu kwa mwarabu , wala mweupe kwa mweusi au mweusi kwa mweupe isipokuwa kwa Taqwa( kumcha Allah).
“Eleweni kila muislamu ni ndugu kwa muislamu na waislamu wote ni ndugu. Hatohalalishiwa muislamu kitu chochote isipokuwa kila alichopewa kwa ridhaa na ndugu yake . Wala msidhulumu nafsi zenu . Na msisahau kwamba kuna siku mtakutana na mola wenu na mtahesabiwa amali zenu. Hivyo tahadharini msije mkapotea baada yangu”
“Enyi watu ! Hakuna tena Mtume baada yangu na hakuna dini nyengine itakayokuja. Ninakuachieni vitu viwili ambavyo mkishikamana navyo hamtopotea milele navyo ni QURAAN na SUNNA (mwenendo) zangu.”
“Wale wote walionisikiliza waufikishe ujumbe huu kwa wengine, na wengine waufikishe kwa watakaofuatia na inawezekana hawa wa mwisho wakayafahamu vyema maneno yangu kuliko hawa walionisikiliza moja kwa moja.”

“Ewe mola shuhudia kwamba nimefikisha ujumbe kwa watu wako”

Ndugu zangu waislamu, hazina kama hizi ndizo tulizoagizwa kufikishiana. Inshaallah kila atakaepata ujumbe huu ahakikishe anamfikishia mwengine kama tulivyoagizwa na Al Habib Mustafa (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) na asaa inawezekana miongoni mwetu kuwapata tutakaomsikiliza Mtume(Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) na kumfahamu vyema na hivyo kuufuata mwenendo wake . Tumuombe Allah(Subhaanahu Wata’ala) atujaalie miongoni mwao. Amin

No comments:

Post a Comment

Animated Social Gadget - Blogger And Wordpress Tips Twitter Bird Gadget