Thursday, April 26, 2012

Kwanini mnakanusha UTATU Mtakatifu?

Swali:
Mimi Mkatoliki ninaamini Mungu ni mmoja. Katika huyu Mungu mmoja, tuna UTATU MTAKATIFU (Holly Trinity), Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Ni Mungu mmoja, nafsi tatu .
Je kwanini ninyi waislamu mnapotajiwa Utatu mtakatifu mnakanusha kwa jazba?


Jibu:
Kwa kuwa ninatambua na kuheshimu imani ya dini nyingine, sina haja ya kukanusha juu ya wewe kuamini uwepo wa Mungu mmoja kwa nafsi tatu..

Naomba niichambue katika uelewa wangu juu ya imani kuwa Baba, Mwana na Roho Mtakatifu ni mmoja. 
Mt Paulo katika barua yake ya kwanza kuwapelekea Wakorintho aliandika:
Naam, na sisi tumeonekana kuwa mashahidi wa uongo wa Mungu; kwa maana tulimshuhudia Mungu ya kuwa alimfufua Kristo, ambaye hakumfufua, ikiwa wafu hawafufuliwi.
1 Wakorintho 15.15
Juu ya kuwa Paulo anaambiwa ya kuwa akiamini kuwa Masihi (yaani Kristo) na Mwenyezi Mungu ni kitu kimoja hapa anasema: "Tulimshuhudia Mungu ya kuwa alimfufua Kristo." Ikiwa Mungu kamfufua Kristo, hawawezi kuwa wote wawili hao ni mtu mmoja. Mmoja alikuwa ni mtenda, mfufuaji, na wa pili alikuwa ni mtendwa, mfufuliwa. 

Kama Kristo ni Mungu mwenye uwezo wa kufufua basi maelekeo ni kusema: "Kristo kajifufua", sio kafufuliwa. Mwenye kufufuliwa ni mfu asiyejiweza kitu. 
Katika kitabu cha Matendo ya Mitume inasimuliwa kuwa Mt Stefano alisema aliyoyaona yaliyo mbinguni. Alisema:
Tazama! naona mbingu zimefunguka, na Mwana wa Adamu amesimama mkono wa kuume wa Mungu.
Matendo 7.56
Mwana wa Adamu ndiye Yesu, na kwa jina hilo ndio mwenyewe akipenda kujiita, sio Mwana wa Mungu. Hapo basi huko mbinguni Stefano anasema anamwona Yesu kakaa mkono wa kulia wa Mungu. Mwenye kukaa mkono wa kulia wa fulani hawezi kuwa ndiye yule yule fulani. 

Hayo ni maelezo ya mbinguni. Ni wazi basi kwa ushahidi wa Biblia kuwa Yesu hakuwa Mungu mbinguni kama alivyokuwa si Mungu duniani. 
Yesu alipokimbilia kwenye Mlima wa Zaituni na huku akisakwa na Mayahudi alijitenga na wanafunzi wake. Huko faraghani aliomba hivi:
Ee Baba, ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki; walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke. Malaika kutoka mbinguni akamtokea akamtia nguvu.
Luka 22.42-43
Hapa tunaona mambo matatu muhimu:
1. Yesu anamwomba Mungu. Yesu anamwabudu Mungu. Wawili hao ni mbali mbali, na vyeo vyao ni mbali mbali. Yesu ni mtumwa mnyonge mwenye kuomba na kuabudu. 

Na Mungu ni Mwenyezi Mungu mwenye uwezo wote na mwenye kustahiki kuabudiwa pekee, hata na Yesu, mwenye kutakiwa msaada pekee, hata na Yesu.
2. Mapenzi ya Mungu ni mbali na yale ya Yesu. Yesu hataki kuuliwa, ananyenyekea na kuomba kwa Bwana wake: "uniondolee kikombe hiki" cha mauti. Yesu hana azma hata chembe ya kufa msalabani, kifo cha mhalifu, kifo cha laana kama maadui zake Mayahudi walivyoazimia kumpatilisha nacho. Lakini anakiri kuwa ni mapenzi ya Mungu sio yake yeye yatendeke. Yeye hana hila wala nguvu za kuzuia kudra ya Mwenyezi Mungu.
3. Yesu, Mwana wa Adamu, anakata tamaa. Imani inampunguka. 

Kavunjika moyo. Ikabidi "Malaika kutoka mbinguni akamtokea akamtia nguvu."
Jee, yaelekea kuwa Yesu ndiye Mungu? Yaelekea kuwa yeye na Mungu kuwa ni sawa? Kama upo wasiwasi wo wote wa kujibu hayo, mwenyewe Yesu anajibu kama anavyo hadithiwa na Yohana kuwa kasema:
Baba ni mkuu kuliko mimi.
Yohana 14.28
Na mwishoni naye yupo mslabani:
Na kama saa tisa, Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu akisema, Eloi, Eloi, lama sabakthani? yaani, Mungu wangu, Mungu wangu, Mbona umeniacha?
Mathayo 27.46
Yafaa hapa tujiulize: Yesu akimlilia Mungu gani hapo msalabani ikiwa naye mwenyewe ni Mungu? Au nini alikusudia aliposema: "Mungu wangu naye ni Mungu wenu"? Maneno hayo kama yanaonyesha cho chote basi yanaonyesha unyenyekevu wa Yesu mbele ya Mungu wake. 

La kustaajabisha ni kule kukata tamaa kwake na kuvunjika moyo. Huwaje mtu wa imani, licha ya nabii na mwana pekee wa Mungu, akate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu. Ama kuwa Mungu akate tamaa na Mungu, na kumyayatikia: "Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha", ni jambo ambalo halimkiniki kuwa. 
Kwa uthibitisho ulio wazi Biblia inatwambia kuwa Yesu si Mungu, wala Mungu si Yesu.

Pia naomba nikujulishe juu ya imani yetu katika haya; 
1-Kuwa mungu ni mmoja – Katika Quran 112:1
2-Roho Mtakatifu – Katika imani yetu roho mtakatifu ni malaika Jibril (Gabriel) ambaye Mwenyezi Mungu anatujuza katika Quran 5:110 Mungu anasema “ Na pale Mwenyezi Mungu atapo sema: Ewe Isa bin Maryamu! Kumbuka neema yangu juu yako, na juu ya mama yako, nilipo kutia nguvu kwa Roho Takatifu (Jibril), ukazungumza na watu katika utoto na utuuzimani. Na nilivyo kufunza kuandika na hikima na Taurati na Injili. 

Na ulipo tengeneza udongo sura ya ndege, kwa idhini yangu, kisha ukapuliza ikawa ndege kwa idhini yangu; na ulipo waponesha vipofu na wakoma kwa idhini yangu; na ulipo wafufua wafu kwa idhini yangu; na nilipo kukinga na Wana wa Israili ulipo wajia na hoja zilizo wazi, na wakasema walio kufuru miongoni mwao: Haya si lolote ila ni uchawi mtupu!
3-Yesu kristo – Nabii Issa, ukiangalia Quran 5:75. Mungu anatujuza kuwa “Masihi mwana wa Maryam si chochote ila ni Mtume. Wamekwisha pita Mitume kabla yake. 

Na mama yake ni mwanamke mkweli. Wote wawili walikuwa wakila chakula. Angalia jinsi tunavyo wabainishia Aya, kisha angalia vipi wanavyo geuzwa. (Na yeye na mwanawe, Isa, walikuwa wana mahitajio yanayo hitajiwa na kila mwanaadamu, kama kula na kunywa, na kwenda haja. Na hizo ni dalili za ubinaadamu wao. Basi hebu zingatia, ewe mwenye kusikia, hali ya hao walio ingia upofu hata hawaoni dalili za Ishara zilizo wazi ambazo amewabainishia Mwenyezi Mungu. Tena zingatia vipi wanaiacha Haki juu ya kuwa ni iwazi kabisa.)
Uthibitisho wa Utatu Mtakatifu: Nianze na Mwanzo 1:26“Na tufanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu, nao watawale samaki wa baharini na viumbe vinavyoruka vya mbinguni na wanyama wa kufugwa na dunia yote na kila mnyama anayetembea juu ya dunia.”
Tufanye, wetu, yetu = Je, unafikiri Mungu anamwambia nani tufanye, sura yetu na mfano wetu?
Kuhusu hili, Mwenyezi Mungu anakanusha kwa kusema katika Quran 112:4 kuwa “Wala hana anaye fanana naye hata mmoja.”
(hapa nikukumbushe kuwa Adam aliumbwa kwa ufinyanzi wa Mungu kule Eden na binadamu waliobaki walizaliwa kwa zinaa. Ikiwa bikira alishika mimba, unaweza kuniambia huu ni utaratibu gani kati ya namna mbili ambazo binadamu walipatikana?)
Labda katika miujiza yote ya kumthibitishia Yesu ungu ni kule kuzaliwa kwake na bikra bila ya baba. Wengi wanaona hayo ndiyo yanayoonyesha kwa nguvu zaidi kuwa yeye ni Mungu au Mwana wa Mungu. Mtaalamu mkubwa wa Kikristo, Maurice Wiles, Professor of Divinity and Canon of Christ Church Oxford, na Mwenyekiti wa Tume ya Imani ya Kanisa la Kiingereza, ameeleza vipi ilivyokuwa ni muhimu kabisa kuamini kuzaliwa na bikra kwa mwenye kutaka kuamini kwamba Yesu ni Mungu. Professor Wiles akiandika katika kitabu The Myth of God Incarnate (Uwongo wa Mungu kuwa Mtu) amesema:
"Mwanzoni mwa karne hii (ya ishirini) zilipokuwa shaka shaka zinatamkwa kuwa ati ni kweli hakika Yesu alichukuliwa mimba na bikra, maneno hayo ya kuonyesha shaka yalionekana mara nyingi kuwa ni mashambulio khasa juu ya imani ya kuwa Mungu kawa mtu. Ilionekana kwamba imani ya kuzaliwa na bikra na kwamba Mungu amekuwa mtu ni kama pacha wasiobandukana, ama zitasimama pamoja au zianguke pamoja."

Biblia yasemaje juu ya jambo hili? Kwa hakika si kitu cha kawaida mtu kuzaliwa na mwanamke bikra asiyeingiliwa. Ni kweli huo ni muujiza. Lakini ndio ndivyo kuamini kuwa chenye kuzaliwa kwa muujiza ni Mungu? Au hata ndio ndivyo kuona tukio kama hilo ni dalili mojawapo ya kuzidisha ushahidi ya kuwa huyo mtoto ni Mungu au Mwana wa Mungu, kwa maana wanavyotaka wakuu wa makanisa wafwasi wao waamini? 
Biblia inayotwambia kuwa Yesu kazaliwa bila ya mama yake kuingiliwa na mwanaadamu (Injili ya Mathayo 1.18) vile vile inatuambia ya kuwa Adamu hakuwa na baba wala mama. (Mwanzo 1.26- 27). Kama wa Yesu ni muujiza wa Adam ni muujiza mardufu. Hali kadhaalika Paulo amewaandikia Waebrania:
Kwa maana Melkizedeki huyo, mfalme wa Salemu, kuhani wa Mungu aliye juu, aliyekutana na Ibrahimu alipokuwa akirudi katika kuwapiga hao wafalme, akambariki; ambaye Ibrahimu alimgawia sehemu ya kumi ya vitu vyote; (tafsiri ya jina lake kwanza ni mfalme wa haki, tena mfalme wa Salemu, maana yake, mfalme wa amani; hana baba, hana mama, hana wazazi, hana mwanzo wa siku zake, wala mwisho uhai wake, bali amefananishwa na Mwana wa Mungu); huyo adumu kuhani milele.
Waebrania 7.1-3
Tunaona basi Biblia inatuhakikishia kuwa Yesu hakuwa pekee mwenye kuzaliwa bila ya baba. Wapo waliomtangulia katika muujiza huu. Kama huo ndio ungu, basi wangelikuwa Adam na Melkizedeki wa mbele, ambaye anasimuliwa na Biblia kuwa alikuwa
"hana baba, hana mama, hana mwanzo wala mwisho".

Hoja nyingi zimetolewa kukanya fikra ya kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu aligeuka binaadamu akaishi duniani kwa sura ya Yesu wa Nazareti. Hoja hizo ziko za misahafuni mpaka za kisayansi. Katika Qur'ani ameshabihishwa Yesu na Adam. Hali kadhaalika muujiza ulitokea kabla kidogo tu ya kuzaliwa Yesu, alipochukua mimba Elizabeti, mke wa Zakaria na ilhali huyo mama ni tasa tangu ujana wake na hapo kesha zeeka na kapindukia miaka ya kuzaa. Mumewe, naye, Zakaria alikuwa ni mkongwe. Mwenyezi Mungu amesema katika Qur'ani, Sura ya Al Imran:
Akasema Zakaria: Mola wangu! Vipi nitapata mtoto, na hali ukongwe umesha nifika, na mke wangu ni tasa? Mwenyezi Mungu akasema: Ndivyo vivyo hivyo, Mwenyezi Mungu hufanya apendavyo.
(Qur'ani) Al Imran 3.40
Ilipofika zamu ya Maryam kuchukua mimba Qur'ani inasema:
(Maryam) akasema: Mola Mlezi wangu! Vipi nitampata mtoto na hali hajanigusa mwanaadamu ye yote? (Mwenyezi Mungu) akasema: Ndivyo vivyo hivyo, Mwenyezi Mungu huumba apendacho; anapohukumu jambo, huliambia: Kuwa! Basi likawa.
(Qur'ani) Al Imran 3.47
Hizi ni hoja za misahafu, ni hoja za watu wenye imani. Wapo wengineo ambao wamepuuzilia mbali hadithi yote hiyo ya kuwa Maryam kachukua mimba bila ya kuingiliwa na mtu. Hao ni kama Mayahudi ambao wanamtukana Yesu na mama yake kwa kusema kuwa hiyo ni mimba ya haramu. Miongoni ya wataalamu wa Kizungu wenye asli ya Ukristo wapo wanaoamini hayo. Wanasema kuwa imani ya kuzaliwa na mama bikra ilikuwako tangu zamani katika dini za kipagani (kishirikina) kabla ya kuja Yesu. Bikra Rea Silvia alimzaa Romulus wa Roma. Horus wa Misri alizaliwa na Isis, malkia bikra wa mbinguni. Hoja inayotolewa kama ilivyokuwa hizi na nyenginezo ni hadithi za kubuni tu zilioenea pande za Bahari ya Kati, basi ndio hivyo hivyo hadithi ya kuwa Maryam alikuwa bikra alipochukua mimba na kumzaa Yesu ni hadithi ya kubuni kuiga zile zilizotangulia. 
Mtaalamu wa Biblia wa Kitaliana, Marcello Craveri anawashutumu wakuu wa Kanisa kwa kutafuta kila kipengee katika Biblia kutoa ushahidi kuwa kuzaliwa kwa Yesu na bikra kuliaguliwa mbele. Kipande kinachonukuliwa mno ni kile kiliomo katika Isaya ambacho kinasema:
Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara. Tazama, bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli.
Isaya 7.14
Mtaalamu huyu anasema maneno haya hayakukhusu kuzaliwa kwa Yesu hata chembe. Kwanza neno la asli halikutaja "bikira" lakini ni "mwanamke kijana". Tafsiri nyingine kama Revised Standard Version zimefuata hivyo ilivyo asli. Neno la Kiebrania liliotumiwa ni almah ambalo maana yake ni mwanamke kijana au msichana. Neno bikra kwa Kiebrania ni bethulah, kama ilivyo katika Kiarabu batuul. Na haya mambo ambayo yametokea zaidi ya miaka 700 kabla ya Yesu yalikhusiana na mke wake Isaya ambaye alikuwa umri wake ni miaka 20 wakati ule na kweli akaja kumzaa mtoto mwanamume. Ama hilo neno Imanueli, maana yake ni Mwenyezi Mungu yu pamoja nasi, na wala sio maana yake kuwa huyo mtoto kuwa ndiye Mungu. Lugha ya Kiebrania imekaribiana na Kiarabu, na kwa Kiarabu ni Ma'anallah, nalo ni jina la kawaida, na kama kwamba kumwombea kheri huyo mwenye kuitwa. Mtaalamu Isaac Asimov ameeleza wazi juu ya utabiri huu wa Isaya katika kitabu chake, Asimov's Guide to the Bible. 
Mtaalamu mwengine mwenye kupima mambo kiakili aitwaye G. Vermes amesema katika kitabu chake Jesus the Jew(Yesu Myahudi) akidai kuwa hili neno "bikira" hata lilivyotumiwa kwa Mariamu yawezekana sana kuwa maana yake ni kuwa mdogo mno kwa uzazi, kama walivyokuwa Sara, Hanna na Elizabeti kuwa ni wakongwe mno, au tasa. 
Mwishoe kuna maoni ya mwana-sayansi na daktari juu ya hili suala la kushika mimba mwanamke hali naye ni bikra. Dr. T.H. Van de Velde M.D. akiandika katika kitabu chake cha kitaalamu, Ideal Marriage (Ndoa Bora) anasema:
"Mara nyingi imewahi kutokea, ijapokuwa ni nadra, kushika mimba kwa kupenya mbegu ya uzazi katika utupu wa mwanamke bila ya kuingiza kabisa dhakari, au utupu wa mwanamume. Mifano kama hiyo ni muhimu kabisa kimaisha. Ni dhaahiri kuwa inathibitisha vitu viwili. 

Kwanza, kuwa katika hali maalumu yawezekana mimba kutiwa ijapokuwa kizinda hakikupasuliwa. Na pili ya kwamba mbegu ya uzazi yaweza kufika ndani ya utupu wa mwanamke kwa njia isiyokuwa moja kwa moja, kwa mfano kwa mguso wa kidole..."

Hapana shaka pana utaalamu mkubwa katika mawazo na fikra hizi, za kidaktari, za kisayansi au za kiakili; lakini ni Qur'ani ndiyo inauweleza ukweli kwa maneno mepesi kabisa hata watoto wachanga wakaweza kuelewa na ikawa ya kuwatukuza Yesu na mama yake:
Hakika mfano wa Isa kwa Mwenyezi Mungu ni kama mfano wa Adam; alimuumba kwa mchanga kisha akamwambia: Kuwa! Basi akawa. Hii ni kweli inayotoka kwa Mola wako Mlezi. Basi usiwe miongoni mwa wanaofanya shaka.(Qur'ani) Al Imran 3.59-60

No comments:

Post a Comment

Animated Social Gadget - Blogger And Wordpress Tips Twitter Bird Gadget