Wednesday, April 25, 2012

Uislamu katika Biblia


Kuna baadhi ya ndugu zetu wasio waislamu huwa wanauliza juu ya mwingiliano wa Uislamu katika biblia..

Ifuatayo ni baadhi ya mifano ya mafundisho aliyoyafuata nabii Yesu na kuyafundisha, lakini baadaye yaliachwa na Kanisa. Hata hivyo, mengi miongoni mwa mafundisho hayo yalifufuliwa katika ujumbe wa mwisho wa Uislamu ulioletwa na Mtume Muhammad (SAW) na yakaendea kubakia kuwa ni sehemu ya msingi katika matendo ya dini ya Kiislamu hadi leo hii.

Kutahiri

Yesu alitahiriwa. Kwa mujibu wa Agano la Kale, mapokeo haya yalianzia na Mtume Ibrahimu, ambaye yeye mwenyewe hakuwa Myahudi wala Mkristo. Katika Mwanzo 17:10-13, imeandikwa, “Hili ndilo agano langu utakalolishika, kati ya mimi na wewe, na uzao wako baada yako, Kila mwanamume wa kwenu atatahiriwa. Mtatahiriwa nyama ya magovi yenu, na jambo hilo litakuwa ishara ya agano kati ya mimi na nyinyi. Mtoto wa siku nane atatahiriwa kwenu, kila mwanamume katika vizazi vyenu, mzaliwa nyumbani, na mnunuliwa kwa fedha, kila mgeni asiyekuwa wa uzao wako. Mzaliwa nyumbani mwako, na mnunuliwa na fedha yako, lazima atahiriwe; na agano langu litakuwa katika mwili wenu, kuwa agano la milele.
Katika Injili kwa mujibu wa Luka 2:21: “Hata zilipotimia siku nane za kumtahiri, aliitwa jina lake Yesu; kama alivyoitwa na malaika kabla hajachukuliwa mimba.” Kwa hiyo, kutahiriwa ilikuwa ni sehemu ya njia ya Yesu. Hata hivyo, leo hii Wakristo wengi hawajatahiriwa, kwa sababu ya mantiki iliyoletwa na Paulo. Yeye alidai kuwa kutahiriwa kulikuwa ni kutahiriwa kwa moyo. Katika waraka wake kwa Warumi 2:29, ameandika: Bali yeye ni Myahudi aliye Myahudi kwa ndani; na tohara ni ya moyo, katika roho, si katika andiko;..." Na katika waraka wake kwa Wagalatia 5:2, ameandika “Tazama, mimi Paulo nawaambia ninyi ya kwamba, mkitahiriwa, Kristo hatawafaidia neno.”[1] Hii ni tafsiri isiyo ya kweli ya Paulo. Kwa upande mwingine, Yesu hakutahiriwa moyoni wala hajasema lolote juu ya kutahiriwa moyoni; yeye aliliendeleza "agano la milele" na alitahiriwa katika nyama. Kwa hiyo, sehemu muhimu ya kufuata njia ya Yesu ni kutahiriwa. Mtume Muhammad (SAW) amenukuliwa akisema: "Mambo matano ni katika maumbile,[2]  kutahiri, kunyoa nywele za sehemu za siri, kunyoa nywele za kwapani, kukata kucha, na kupunguza masharubu." Imepokewa na Bukharin na Muslim." [3]

Nguruwe

Yesu hajakula nguruwe. Alifuata sheria za Musa na hakula nguruwe. Katika Walawi 11:7-8, “Na nguruwe, kwa sababu yeye anazo kwato, ni mwenye miguu iliyopasuka kati, lakini hacheui, yeye ni najisi, kwenu, msiile nyama yao, wala msiiguse mizoga yao; hao ni najisi kwenu.”[4]
Yesu alishughulika na nguruwe pale tu, alipowaruhusu pepo wabaya waliomwingia mtu wawaingie nguruwe. Na walipoliingia kundi la nguruwe, hao nguruwe walikimbilia kwenye maji na kuzama. 
Hata hivyo, watu wengi wanaojiita Wakristo leo hii sio tu wanakula nguruwe, lakini pia wanampenda sana kiasi cha kumfanya nguruwe kuwa mada ya wimbo wa chekechea [mfano wimbo: Huyu Nguruwe Mdogo alienda sokoni…] na hadithi za watoto [mfano: Nguruwe Wadogo Watatu]. Nguruwe na Nyama ya nguruwe ni wahusika mashuhuri wa katuni, na hivi karibuni hadithi ya sinema ndefu imetayarishwa kuhusu nguruwe aitwaye "Babe". Kwa hiyo, inawezekana kusema kuwa wale wanaojiita ni wafuasi wa Kristo kwa hakika hawafuati njia ya Kristo.
Katika sheria ya Kiislamu, kuharamishwa kwa nguruwe na mazao yake kumetekelezwa kwa nguvu tangu wakati wa Mtume Muhammad (SAW) hadi leo hii. Katika Quran, Sura ya Al-Baqarah 2:173, Mungu anasema:
"إِنَّمَا حَرَّمَ عَلَيْكُمُ الْمَيْتَةَ وَالدَّمَ وَلَحْمَ الْخِنزِيرِ وَمَا أُهِلَّ بِهِ لِغَيْرِ اللّهِ فَمَنِ اضْطُرَّ غَيْرَ بَاغٍ وَلاَ عَادٍ فَلا إِثْمَ عَلَيْهِ إِنَّ اللّهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ"
"Yeye amekuharimishieni mzoga tu na damu na nyama ya nguruwe na kilichotajiwa, katika kuchinjwa kwake, jina la asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Lakini aliyefikiwa na dharura bila ya kutamani wala kupita kiasi, yeye hana dhambi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu." Al-Baqarah 2:173 [5]

Damu

Pia, Yesu hakula kitu chochote cha damu, wala hajakula damu. Mungu amenukuliwa akimfundisha Mtume Musa katika Torati, Kumbukumbu la Torati 12:16, “Lakini msiile damu; imwageni juu ya nchi kama maji.”. Na katika Lawi 19:26, “Msile kitu cho chote pamoja na damu yake; wala msifanye kuloga, wala kutumia utambuzi.” Katazo hili limelindwa hadi leo hii katika ufunuo wa mwisho katika Sura Al-Anaam 6:145
"قُل لاَّ أَجِدُ فِي مَا أُوْحِيَ إِلَيَّ مُحَرَّمًا عَلَى طَاعِمٍ يَطْعَمُهُ إِلاَّ أَن يَكُونَ مَيْتَةً أَوْ دَمًا مَّسْفُوحًا أَوْ لَحْمَ خِنزِيرٍ فَإِنَّهُ رِجْسٌ..."
"Sema: Sioni katika yale niliyofunuliwa mimi kitu kilichoharimishwa kwa mlaji kukila isipokuwa kiwe ni nyamafu, au damu inayomwagika, au nyama ya nguruwe, kwani hiyo ni uchafu;…" Al-Anaam 6:145
Hivyo, ibada maalum ya kuchinja ilifanywa iwe sheria na Mungu kwa mataifa yote yaliyopelekewa mitume, ili kuhakikisha kuwa damu nyingi inaondoshwa kwa ufanisi kutoka kwa mnyama aliyechinjwa na kumkumbusha mwanadamu fadhila za Mungu. Quran inataja mafundisho haya katika sura ya Al-Hajji 22:34 kama ifuatavyo:
"وَلِكُلِّ أُمَّةٍ جَعَلْنَا مَنسَكًا لِيَذْكُرُوا اسْمَ اللَّهِ عَلَى مَا رَزَقَهُم مِّن بَهِيمَةِ الْأَنْعَامِ..."
"Na kila umma tumewafanyia mahala pa kuchinjia mihanga ya ibada ili walitaje jina la Mwenyezi Mungu juu ya vile walivyoruzukiwa katika wanyama wa mifugo…" Al-Hajji 22:34
Yesu na wafuasi wake wa kwanza waliuona mfumo mkamilifu wa kuchinja kwa kutaja jina la Mungu na kukata mishipa ya shingo ya mnyama akiwa hai ili kuuruhusu moyo usukume nje damu. Hata hivyo, Wakristo wa leo hii hawaambatanishi sana umuhimu wa mfumo wa kuchinja kikamilifu, kama ulivyofanywa sheria na Mungu.

Kilevi (pombe)

Yesu aliitoa nafsi yake kwa ajili ya Mungu na kwa hiyo alijizui na vinjwaji vya kulevya kwa mujibu wa mafundisho yaliyorekodiwa katika Hesabu 6:1-4 “Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia, Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Mtu mume au mke atakapoweka nadhiri kubwa, nadhiri ya Mnadhiri, ili ajiweke wakfu kwa BWANA; atajitenga na divai na vileo; hatakunywa siki ya divai, wala siki ya kileo, wala asinywe maji yoyote ya zabibu, wala asile zabibu mbichi wala zilizokauka. Siku zote za kujitenga kwake asile kitu cho chote kilichoandaliwa kwa mzabibu, tangu kokwa hata maganda." ”.[6]
Katika Quran, Sura Al-Maaidah 5:90, Allah anaharamisha kileo bila kubadilika.
"يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ إِنَّمَا الْخَمْرُ وَالْمَيْسِرُ وَالأَنصَابُ وَالأَزْلاَمُ رِجْسٌ مِّنْ عَمَلِ الشَّيْطَانِ فَاجْتَنِبُوهُ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ"
"Enyi mlio amini! Bila ya shaka ulevi, na kamari, na kuabudu masanamu, na kupiga ramli, ni uchafu katika kazi ya Shet'ani. Basi jiepusheni navyo, ili mpate kufanikiwa." Al-Maaidah 5:90
Na ule muujiza wa 'kugeuza maji yawe pombe',[7] unaopatika katika Injili ya Yohana tu, na ambao mtiririko wake unapingana na Injili nyingine. Kama ilivyotajwa mwanzoni, Injili ya Yohana ilipingwa ikiwa kama uasi katika kanisa la kwanza,[8] huku Injili tatu zilizobakia zimetajwa kama ni muhtasari wa Injili kwa sababu maandiko yaliyomo ni sawa na matendo ya maisha ya Yesu.[9] Hivyo, wasomi wa Agano Jipya wameonyesha shaka juu ya uhalisia wa utunzi wa tukio hili.

Udhu kabla ya Kusali

Kabla ya kusali kikawaida, Yesu aliosha viungo vyake kwa mujibu wa mafundisho ya Torati. Musa na Haruna wamenukuliwa wakifanya hayo hayo katika Kutoka 40:30-31, “Akaliweka birika kati ya hema ya kukutania na madhabahu, akatia maji ndani yake ya kuoshea. Musa na Haruni, na wanawe wakanawa mikono yao na miguu yao ndani yak.”
Katika Quran, Sura Al-Maaidah, 5:6, udhu kwa ajili ya sala umefanywa kuwa ni sheria na lazima kama ifuatavyo:
"يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ إِذَا قُمْتُمْ إِلَى الصَّلاةِ فاغْسِلُواْ وُجُوهَكُمْ وَأَيْدِيَكُمْ إِلَى الْمَرَافِقِ وَامْسَحُواْ بِرُؤُوسِكُمْ وَأَرْجُلَكُمْ إِلَى الْكَعْبَينِ..."
"Enyi mlioamini! Mnaposimama kwa ajili ya Sala basi osheni nyuso zenu, na mikono yenu mpaka vifundoni, na mpake vichwa vyenu, na osheni miguu yenu mpaka vifundoni…" Al-Maaidah, 5:6

Kusujudi katika Sala

Yesu ameelezwa katika Injili kuwa amesujudi alipokuwa akisali. Katika Mathayo 26:39, mtunzi anaeleza tukio lililotokea pale Yesu alipoenda na wanafunzi wake hadi Gethsemane: “Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifulifuli, akaomba, akasema, Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke; walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utavyo wewe.”
Wakristo wa leo hii wanapiga magoti, wanakutanisha viganja vyao, katika mkao ambao hauwezi kuwa ndio sheria ya Yesu. Mfumo wa kusujudu katika sala uliofuatwa na Yesu haukuwa wa kujifanyia mwenyewe. Ulikuwa ndio mtindo wa sala wa manabii wa kabla yake. Katika Agano la Kale, Mwanzo 17:3, Nabii Ibrahimu anarekodiwa kuwa alianguka juu ya uso wake katika sala; katika Hesabu 16:22 na 20:6, wote wawili Musa na haruna wamerekodiwa kuwa wameanguka juu ya nyuso zao katika kuabudu; katika Yoshua 5:14 na 7:6, Yoshua alianguka juu ya uso wake ardhini na aliabudu; katika 1 Wafalme 18:42, Eliya alisujudu ardhini na kuweka uso wake kati ya magoti yake. Hii ilikuwa njia ya mitume ambayo kupitia kwao Mungu amechagua kufikisha neno Lake duniani; na kwa njia hii tu, wale wote wanaodai kumfuata Yesu watapata uwokovu aliouhubiri katika Injili.
Sura ya Al-Insaan 76:25-6, ni mfano mmoja tu katika mifano mingi ya Quran juu ya mafundisho ya Mungu kwa waumini wasujudu wanapomuabudu.
"وَاذْكُرِ اسْمَ رَبِّكَ بُكْرَةً وَأَصِيلًا، وَمِنَ اللَّيْلِ فَاسْجُدْ لَهُ وَسَبِّحْهُ لَيْلًا طَوِيلًا"
"Na likumbuke jina la Mola wako Mlezi asubuhi na jioni; Na usiku msujudie Yeye, na umtakase usiku, wakati mrefu." Al-Insaan 76:25-6

Hijabu

Wanawake waliomzunguka Yesu walivaa hijabu kulingana na matendo ya wanawake waliokuwa karibu na mitume ya mwanzo. Nguo zao zilikuwa ni pana na za kufunika mwili wao wote, na walivaa ushungi unaofunika nywele zao. Katika Mwanzo 24:64-5: “Rebeka akainua macho, naye alipomwona Isaka, alishuku juu ya ngamia. Akamwambia mtumishi, Ni nani mtu huyu ajaye kondeni kutulaki? Mtumishi akasema, Huyu ndiye bwana wangu. Basi akatwa shela yake akajifumika.” Paulo ameandika katika waraka wake kwa 1 Wakorinto 11:5-6, Bali kila mwanamke asalipo, au anapohutubu, bila kufunikwa kichwa, yuaaibisha kichwa chake; kwa maana ni sawasawa na yule aliyenyolewa. Maana mwanamke asipofunikwa na akatwe nywele. Au ikiwa ni aibu mwanamke kukatwa nywele zake au kunyolewa, na afunikwe.” Kuna wanaoweza kupinga na kudai kuwa hilo lilikuwa ni mila ya wakati huo kujifunika mwili mzima. Hata hivyo, hiyo sio hoja. Katika sehemu zote Roma na Ugiriki, ambao utamaduni wao ndio ulikuwa ukiongoza eneo hilo, vazi la wengi lilikuwa ni fupi hasa na kuonyesha mikono, miguu, na kifua. Ni wanawake wa Kipalestna wanaofuata dini tu, wakifuata mapokeo ya Kiyahudi, ndio waliojifunika kwa kujistiri.
Kwa mujibu wa Rabbi Dr. Menachem M. Brayer (Profesa wa Biblical Literature wa Chuo Kikuu cha Yeshiva), Ilikuwa ni mila kuwa wanawake wa Kiyahudi kutoka nje kwenye watu wengi wakiwa wamefunika vichwa, na wakati mwingine wanafunika uso mzima, na kuacha jicho moja tu.[10] Ameendelea kueleza zaidi kuwa "katika kipindi cha Tannaitic, mwanamke wa Kiyahudi atakayeshindwa kufunika kichwa chake alichukuliwa kuwa anafedhehesha utu wake. Na kichwa chake kinapokuwa kimefunuka anapaswa apigwe faini ya zumzim mia kwa kosa hilo.[11]
Mwanatiolojia mashuhuri wa Kikristo wa mwanzo, Mtakatifu Tertullian (d. 220 CE), katika pendekezo lake maarufu, 'Juu ya Hijabu ya Mabikira'  ameandika, "Wasichana, vaeni hijabu zenu nje huko mitaani, pia mzivae kanisani; mzivae mnapokuwa na wageni, kisha zivaeni mkiwa na kaka zenu…" Miongoni mwa sheria za kanisa la Katoliki hadi leo hii, kuna sheria inayowataka wanawake wafunike vichwa vyao wakiwa kanisani.[12] Madhehebu ya Kikristo, kama vile Waamish na Wamenonites, wanawake wao waneendelea kuvaa hijabu hadi leo.
Katika Quran, Sura An-Nuur 24:31, waumini wanawake wanaagizwa wafunike mapambo yao na wavae hijabu kichwani na vifuani mwao.
"وَقُل لِّلْمُؤْمِنَاتِ يَغْضُضْنَ مِنْ أَبْصَارِهِنَّ وَيَحْفَظْنَ فُرُوجَهُنَّ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا وَلْيَضْرِبْنَ بِخُمُرِهِنَّ عَلَى جُيُوبِهِنَّ..."
"Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao, wala wasionyeshe uzuri wao isipokuwa unaodhihirika. Na waangushe shungi zao juu ya vifua vyao, …" An-Nuur 24:31
Katika Sura ya Al-Ahzaabu 33:59, lengo la kuvaa hijabu limetolewa. Allah anaeleza kuwa hijabu inawafanya waumini wanawake wajulikane katika jamii na kupata kinga dhidi ya uwezekano wa kudhuriwa na jamii.

Salamu

Yesu aliwasalimia wafuasi zake kwa kusema, "Amani iwe kwenu". Katika Sura 20:19, mtunzi asiyejulikana wa Injili ya Yohana ameandika yafuatayo kuhusu Yesu baada ya dai la kusulubiwa: “Akaja Yesu, akasimama katikati akawaambia, Amani iwe kwenu.” Salamu hii ilikuwa ni kama zile za manabii, kama ilivyotajwa katika vitabu vya Agano la Kale. Kwa mfano, katika 1 Samweli 25:6, Nabii Daudi amewaaagiza wajumbe aliowapeleka kwa Nabal: “Na hivi ndivyo mtakavyomwambia huyu aishiye salama, Amani iwe kwenu”. Quran inawaagiza wale wote wanaoingia katika majumba watoe salamu ya amani;[13] na wale watakaoingia Peponi watasalimiwa hivyo hivyo na malaika.[14] Katika Sura Al-Anaam 6:54, Mungu anawaagiza waumini wasalimiane wao kwa wao kwa amani:
"وَإِذَا جَاءكَ الَّذِينَ يُؤْمِنُونَ بِآيَاتِنَا فَقُلْ سَلاَمٌ عَلَيْكُمْ..."
"Na wanapokujia wanaoziamini Ishara zetu waambie: Assalamu alaikum! Amani iwe juu yenu!..." Al-Anaam 6:54

Zaka

Yesu aliimarisha taasisi ya zaka za lazima, ijulikanayo kama "moja ya kumi", iliyokuwa inachukuliwa kutoka katika mavuno ya kila mwaka na kurejeshwa kwa Mungu kwa sherehe. Katika Kumbukumbu la Torati 14:22: “Usiache kutoa zaka ya fungu la kumi katika maongeo yote ya mbegu zako, yatokayo shamba mwaka baada ya mwaka.”
Katika Sura ya sita, Al-Anaam, aya ya 141, Mungu anawakumbusha waumini walipe zaka wakati wa mavuno:
"وَهُوَ الَّذِي أَنشَأَ جَنَّاتٍ مَّعْرُوشَاتٍ وَغَيْرَ مَعْرُوشَاتٍ وَالنَّخْلَ وَالزَّرْعَ مُخْتَلِفًا أُكُلُهُ وَالزَّيْتُونَ وَالرُّمَّانَ مُتَشَابِهًا وَغَيْرَ مُتَشَابِهٍ كُلُواْ مِن ثَمَرِهِ إِذَا أَثْمَرَ وَآتُواْ حَقَّهُ يَوْمَ حَصَادِهِ وَلاَ تُسْرِفُواْ إِنَّهُ لاَ يُحِبُّ الْمُسْرِفِينَ"
"Na Yeye ndiye aliyeziumba bustani zenye kutambaa juu ya chanja, na zisizotambaa, na mitende, na mimea yenye matunda mbalimbali, na mizaituni na mikomamanga inayofanana na isiyofanana. Kuleni matunda yake inapozaa, na toeni haki yake siku ya kuvunwa kwake. Wala msitumie kwa fujo. Hakika Yeye hawapendi watumiayo kwa fujo." Al-Anaam 6:141[15]
Mfumo wa zaka (kwa Kiarabu, zakaah) umepangwa vizuri, kwa viwango tofauti tofauti kwa pesa na vito vya thamani na vile vya mazao ya kilimo na mifugo. Pia, wote wanaofaa kuipokea wametambulishwa kwa uwazi katika Quran, Sura ya At-Tawbah 9:60. kimsingi inagawanywa miongoni mwa makundi mbalimbali ya maskini na haitumiki katika kuwapa maisha ya anasa viongozi wa kidini.

Kfunga

Kwa mujibu wa Injili, Yesu alifunga kwa siku arobaini. Mathayo 4:2 “Akafunga siku arobaini mchana na usiku, mwisho akaona njaa.”.[16] Hili lilikuwa linalingana na matendo ya manabii wa mwanzo. Pia Musa amerekodiwa katika Kutoka 34:28, kuwa alifunga: “Naye alikuwa huko pamoja na BWANA siku arobaini na masiku yake; hakula chakula, wala hakunywa maji. Naye akaandika katika hizo mbao, hayo maneno ya maagano, hizo amri kumi.”
Katika Quran, Sura Al-Baqarah 2:183, waumini wameagizwa watekeleze funga.
"يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ"
"Enyi mlioamini! Mmeandikiwa Saumu, kama waliyoandikiwa walio kuwa kabla yenu ili mpate kumcha mungu." Al-Baqarah 2:183
Lengo la kufunga limefafanuliwa kwa uwazi nalo ni kendeleza uchamungu. Ni Mungu pekee ajuaye ni nani afungaye kweli na nani hafungi. Hivyo, mfungaji anajizuia na kula, kunywa kwa kutegemea Mungu yu macho. Funga inanyanyua mwamko unaopelekea kupenda sana mema.
Waumini wanapaswa wafunge kuanzia alfajiri hadi kuzama kwa jua katika mwezi mzima wa Ramadhani (mwezi wa tisa wa kalenda ya Kiislmamu ya miezi miandamo). Mtume Muhammad (SAW) pia amesema, "Hakika ya  funga bora ni funga ya Daudi, alikuwa akifunga siku moja na kufungulia inayofuata." [17]

Riba

Kwa kukamata sheria, Nabii Yesu pia alipinga kutoa au kupokea riba kwa sababu maandiko ya Torati yanakataza vikali riba. Imenukuliwa katika kumbukumbu la torati 23:19 kuwa, “Usimkopeshe ndugu yako kwa riba; riba ya fedha, riba ya vyakula,[18] riba ya kitu cho chote kikopeshwacho kwa riba;"[19] Pia riba imekatazwa vikali katika sura Al-Baqarah 2:278 ya Quran:
"يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ اتَّقُواْ اللّهَ وَذَرُواْ مَا بَقِيَ مِنَ الرِّبَا إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ"
"Enyi mlioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na acheni riba zilizobakia, ikiwa nyinyi ni Waumini." Al-Baqarah 2:278
Ili kukamilisha takwa hili la Mwenyezi Mungu, Waislamu wamendeleza mfumo mbadala wa Benki, kwa kawaida unajulikana kama 'Benki ya Kiislamu', isiyo na riba.

Mitala (wake wengi)

Hakuna rekodi zinazoonyesha kuwa Nabii Yesu anapinga mitala. Na kama alifanya hivyo, ingeonyesha kuwa analaani matendo ya manabii waliotangulia kabla yake. Kuna mifano mingi ya ndoa za mitala miongoni mwa manabii iliyorekodiwa katika Torati. Nabii Ibrahimu alikuwa na wake wawili, kwa mujibu wa Mwanzo 16:3: “Sarai mkewe Abramu akamtwaa Hajiri Mmisri mjakazi wake, baada ya kukaa Abramu katika nchi ya Kanaani miaka kumi, akampa Abramu mumewe, awe mkewe.” Pia Nabii Daudi, kwa mujibu wa kitabu cha kwanza cha Samweli 27:3, “Daudi akakaa huko Gathi pamoja na Akishi, yeye na watu wake, kila mtu na watu wa nyumbani mwake; Daudi naye alikuwa na wakeze wawili, Ahinoamu wa Yezreeli, na Abigaili wa Karmeli, aliyekuwa mkewe Nabali.” Katika 1 Wafalme 11:3, Suleimani inasemwa kuwa alikuwa na  “…wake mia saba binti za kifalme, na masuria mia tatu; nao wakeze wakamgeuza moyo.” Mototo wa Suleimani, Rehobo'am, pia alikuwa na idadi kubwa ya wake, kwa mujibu wa 2 Nyakati 11:21, “Rehoboamu akampenda Maaka binti Absalomu kuliko wakeze wote na masuria yake; (maana alioa wake kumi na wanane, na masuria sitini, akazaa wana ishirini na wanane na binti sitini).” Kwa hakika, Torati inafafanua sheria ya kugawa mirathi katika hali za mitala. Katika Kumbukumbu la Torati 21:15-16, sheria inasema: “Ikiwa mtu yuna wake wawili, mmoja ampenda, mmoja hampendi, nao wamemzalia watoto, ampendaye na asiyempenda wote wawili; na yule mzaliwa wa kwanza akiwa ni wa mke asiyependwa; ndipo itakapokuwa ya kwamba siku atakayowarithisha wanawe alivyo navyo, asimweke mwana wa ampendaye kuwa mzaliwa wa kwanza mbele ya mwana wa asiyempenda, naye ndiye mzaliwa wa kwanza huyu;” Kikwazo pekee cha mitala kilikuwa ni kukataza kuoa dada ya mkeo awe mke mwenza katika walawi 18:18, “Wala usitwae mwanamke pamoja na nduguye, awe mtesi wake, na kufunua utupu wake, huyo wa pili atakapokuwa yu hai.” Kitabu cha Talmudi kinashauri kuoa mwisho wake wanne kama ilivyokuwa ikitendwa na Nabii Yakobo.[20]
Kwa mujibu wa Padri Eugene Hillman, "Katika Agano Jipya hakuna sehemu yoyote yenye amri iliyowazi ya kuwa ndoa iwe ya mke mmoja au amri yoyote iliyowazi inayokataza mitala."[21] Akaendelea kutilia mkazo ukweli kuwa, kanisa huko Roma lilikataza mitala ili kuafikiana na utamaduni wa Graeco-Roman unaoweka sheria ya mke mmoja tu huku ikisamehe vimada na ukahaba.[22]
Uislamu umeweka mipaka ya mitala kuwa mwisho kuoa wake wanne kwa wakati mmoja na Uislamu umetangaza kuwatendea wake kwa uadilifu kuwa ndio sharti la msingi la mitala. Katika Sura An-Nisaa 4:3, Mungu anaeleza:
"...فَانكِحُواْ مَا طَابَ لَكُم مِّنَ النِّسَاء مَثْنَى وَثُلاَثَ وَرُبَاعَ فَإِنْ خِفْتُمْ أَلاَّ تَعْدِلُواْ فَوَاحِدَةً..."
"…Oeni mnaowapenda katika wanawake, wawili au watatu au wanne. na mkiogopa kuwa hamwezi kufanya uadilifu, basi mmoja tu…" An-Nisaa 4:3


Hitimisho

Kuna Mungu mmoja tu aliyeumba jamii moja ya wanadamu, na akawafikishia ujumbe mmoja: nao ni kutii matakwa ya Mungu – kunakuojulikana kwa Kiarabu kama Uislamu. Ujumbe huo ulipelekwa kwa watu wa kwanza duniani, na kuthibitishwa na manabii wote wa Mungu waliokuja baada yao, zama zote zilizopita. Kiini cha ujumbe wa Uislamu ni kuwa binadamu lazima wamwabudu Mungu mmoja tu kwa kutii Amri zake, na kuacha kuabudu viumbe wa Mungu vikiwa kama njia, umbo au mfumo wowote ule.
Yesu Kristo, amezaliwa na Bikira Maria, amefanya miujiza na kuwaita Waisraeli katika ujumbe ule ule wa kutii (Uislamu), kama walivyofanya manabii wote waliomtangulia. Yesu hakuwa Mungu, wala hakuwa 'Mwana wa Mungu', lakini alikuwa ni Masihi, Mtume wa Mungu mwenye heshima kubwa. Yesu hajawaita watu wamwabudu yeye; kinyume chake, aliwaita wamwabudu Mungu, na yeye mwenyewe pia alimwabudu Mungu. Aliithibitisha sheria za Torati alizozifundisha Nabii Musa; aliishi nazo na kuwaagiza wanafunzi wake wazifuate kwa maelezo mazuri sana. Kabla ya kuondoka kwake, aliwafahamisha wafuasi wake juu ya Nabii wa mwisho, Muhammad wa Arabuni (SAW), atakayekuja baada yake, na kuwaagiza watii mafundisho yake.
Katika vizazi vya baada ya kuondoka kwa Yesu kutoka katika dunia hii, mafundisho yake yaliharibiwa naye akakuzwa na kufikishwa kuwa Mungu. Karne sita baadaye, baada ya kuja kwa Mtume Muhammad (SAW), hatimaye ukweli juu ya Yesu Kristo ukaelezwa upya na kuhifadhiwa milele katika kitabu cha ufunuo wa Mungu cha mwisho, Quran. Zaidi, sheria za Musa, alizozifuata Yesu, zilifunuliwa upya katika mfumo safi na nadhifu, na kutekelezwa katika njia ya maisha iliyowekwa iwe sheria na Mungu ijulikanayo kama Uislamu.
Hivyo, ukweli wa manabii, ujumbe wao wa aina moja, na njia ya maisha waliyoifuata, vinapatikana vikiwa vimehifadhiwa katika dini ya Kiislamu, dini ya pekee iliyoletwa na Mungu kwa ajili ya wanadamu. Na zaidi, leo hii ni Waislamu pekee wanaomfuata kikweli kweli Yesu na mafundisho yake ya kweli. Njia yao ya maisha inaendana sana na njia ya maisha ya Yesu kuliko "Mkristo" yeyote wa siku hizi. Mapenzi na heshima kwa Yesu Kristo ni kipengele cha imani katika Uislamu. Allah amesisitiza umuhimu wa kumwamini Yesu katika sehemu nyingi katika Quran. Kwa mfano, katika Sura An-Nisaai 4:159, Amesema:
"وَإِن مِّنْ أَهْلِ الْكِتَابِ إِلاَّ لَيُؤْمِنَنَّ بِهِ قَبْلَ مَوْتِهِ وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ يَكُونُ عَلَيْهِمْ شَهِيدًا"
"Na hawi katika Watu wa Kitabu ila hakika atamuamini yeye kabla ya kufa kwake. Naye Siku ya Kiyama atakuwa shahidi juu yao." An-Nisaai 4:159

Kurudi kwa Yesu

Ingawa kuna matarajio ya kurudi kwa Yesu, wanayoyasubiri Wakristo, pia hiyo ni sehemu ya imani ya Kiislamu. Hata hivyo, hatorudi kuhukumu dunia kama wanavyoamini Wakristo wa kisasa, kwa sababu hukumu inamilikiwa na Mungu peke yake. Quran inafundisha kuwa Yesu hakuuliwa na Wayahudi, lakini badala yake alinyanyuliwa na Mungu akiwa hai kwenda mbinguni. An-Nisaai 4:157-158:
"وَقَوْلِهِمْ إِنَّا قَتَلْنَا الْمَسِيحَ عِيسَى ابْنَ مَرْيَمَ رَسُولَ اللّهِ وَمَا قَتَلُوهُ وَمَا صَلَبُوهُ وَلَـكِن شُبِّهَ لَهُمْ وَإِنَّ الَّذِينَ اخْتَلَفُواْ فِيهِ لَفِي شَكٍّ مِّنْهُ مَا لَهُم بِهِ مِنْ عِلْمٍ إِلاَّ اتِّبَاعَ الظَّنِّ وَمَا قَتَلُوهُ يَقِينًا،  بَل رَّفَعَهُ اللّهُ إِلَيْهِ وَكَانَ اللّهُ عَزِيزًا حَكِيمًا "
"Na kwa kusema kwao: Sisi tumemuuwa Masihi Isa, mwana wa Maryamu, Mtume wa Mwenyezi Mungu – nao hawakumuuwa wala hawakumsulubu, bali walifananishiwa tu. Na hakika waliokhitalifiana katika haya wamo katika shaka nayo. Wao hawana ujuzi nayo wowote, ila ni kufuata dhana tu. Wala hawakumuuwa kwa yakini. Bali Mwenyezi Mungu alimnyanyua kwake, na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima." An-Nisaai 4:157-158
Miongoni mwa vitu vilivyoripotiwa kuwa Mtume Muhammad (SAW) amevisema kuhusiana na kurudi kwa Nabii Yesu ni vifuatavyo, "Hakutakuwa na Nabii katika yangu na Isa (Yesu), naye atarejea. Na atakaporeja mtamjua. Atakuwa mtu mwenye umbo zuri na ngozi nyekundu na atashuka akiwa amevaa vipande viwili vya shuka. Nywele zake zitaonekana zimelowa, ingawa hazijaguswa na maji. Atapambana na watu ili kuuimarisha Uislamu, atavunja msalaba, ataua nguruwe na kubatilisha kodi ya jizya.[23] Katika wakati wake, Allah ataziangamiza dini zote ispokuwa Uislamu, pia, Masihi Dajjali atauliwa. Isa atakaa duniani kwa miaka arobaini, na atakapokufa, Waislamu watamsalia sala ya maiti." [24]
Kurejea kwa Yesu kutakuwa ni moja ya alama za kufika Siku ya Kiama.



[1] Pia tazama Wagalatia 6:15.
[2] Neno la Kiarabu lililotumika ni fitrah, linalomaanisha 'maumbile'.
[3] Sahih Al-Bukhari, vol. 7, p. 515, no. 777 na sahihi Muslim, vol. 1, p. 159, no. 495.
[4] Pia tazama, Kumbukumbu la Taroti 14:8.
[5] Pia tazama Sura Al-Maaidah, 5:3.
[6] Huyo ni mtu aliyetengana au mtu aliyejitenga, tunza, weka wakfu.
[7] Yohana 2:1-11.
[8] The Five gospels, p. 20.
[9] The New Fncyclopaedia Britannica, vol. 5, p. 379.

[10] The Jewish Woman in Rabbinic Literature, p.230.
[11] Ibid., p. 139.
[12] Clara M. Henning, "Canon Law and the Battle of thae Sexes," in Religion and Sexism, p.272.
[13] Sura An-Nuur 24:27.
[14] Sura Al-Araaf, 7:46.
[15] Moja ya kumi ikiwa shamba limenyeshewa na mvua na moja ya ishirini kama limemwagiliwa.
[16] Pia tazama Mathayo 6:16 na 17:21.
[17] Sahih Al-Bukhari, vol. 3, pp. 113-4, no. 200 n1 Sahih Muslim, vol. 2, p. 565, no. 2595.
[18]  Chakula au utoaji.
[19] Hata hivyo, katika mstari uliofuatia huu, Wayahudi wamefanya kumkopesha kwa riba mtu asiye Myahudi kuwa ni ruhusa:  "Mgeni waweza kumkopesha kwa riba, ila usimkopeshe ndugu yako kwa riba; …" (Kumbukumbu la Torati 23:20).
[20] Women in Judaism, p. 148.
[21] Polygamy Reconsidered, p. 140.
[22] Ibid., p. 17.
[23] Kodi ichukuliwayo kutoka kwa Wakristo na Wayahudi wanaoishi chini  ya utawala wa Kiislamu badala ya zaka (sadaka ya wajibu) na kuhudumia jeshi.
[24] Sunan Abu Dawud, vol. 3, p. 1203, no. 4310 na imesahihishwa katika Saheeh Sunan Abee Dawood, vol. 3, p. 815-6, no. 3635.

2 comments:

  1. Umeela vzr sana lkn umesahau ya kuwa Yesu aliitunza Sabato kama ilivyo andikwa katika Luka 4:6 na Quran 2:65

    ReplyDelete

Animated Social Gadget - Blogger And Wordpress Tips Twitter Bird Gadget