Saturday, April 28, 2012

Kwanini mnadai eti Yesu ndio Issa?

Swali:
Yafuatayo ni maswali mawili yanayoshabihiana, tunayaweka pamoja ili yajibiwe kwapamoja;
(a)Kwanini waislamu mnadai eti Yesu na Issa ni sawa wakati wao ni tofauti kabisa?

(b) Yesu siyo Issa mbona nyie Waislam hiyo dini yenu ina visa sana? Kwani ni lazima Yesu awe Isa ili mfurahi? Huyo Isa aliyezaliwa chini ya mtende ni wenu mkitaka nendeni mkanywe nae chai sie hatumjui huyo.


Jibu:
Ni upotofu wa dhahiri kudai kuwa Nabii Issa au Yesu hawahusiani, kwa kupachika shuhuda zisizohusiana na mada husika. Na baya zaidi ni kule kutumia hoja dhaifu na za uzushi kama alivyofanya wakristo wengi. 

Mara nyingi wakristo hutoa sababu sita, ikiwemo jina, ukoo, kuumbwa, kuzaliwa, Utume na matendo ya Nabii Issa au Yesu (a.s) kama hoja za kutofautisha majina hayo.
Kwanza ningependa ieleweke kwamba hakuna tofauti kati ya Yesu na Issa kama wanavyotaka kupotosha. Ila ninachoweza kukiri hapa ni kwamba "Yesu mfufuka" anayehubiriwa na Bwana Paulo huyo ni tofauti kabisa na Nabii Issa bin Mariamu. Na kwa mtu asiyeelewa vema maandiko kwa hali yoyote ile ndiye anayeweza kuchanganyikiwa juu ya "Yesu sahihi" ambaye ndiye Nabii Issa bin Mariam (a.s.). Na dawa yake ni kukubali kuelimishwa na si kujifanya kujua, matokeo yake ukapotosha ukweli. Hii ni hatari sana! Sasa hebu tuone upotofu wa sababu hizo wanazozitaja za kutofautisha "Yesu na Issa".
JINA
Wakristo wanasema kimatamshi jina "Yesu" kwa Kiarabu ni "Yasu". Hivyo ndivyo aitwavyo na Waarabu Wakristo tangu zama za kabla ya Muhammad na ndivyo aitwavyo ndani ya Injili ya Kiarabu iliyotafsiriwa na Waraqa bin Naufal bin Asad kabla ya Utume wa Muhammad (Sahihi Muslim 1, Hadithi 301). Jina Issa linatokana na jina Ayas lenye maana ya "Wekundu uliozidiana na weupe" (Baidawi, Vol 1 Uk. 160) mwisho wa kukunuu.
Jibu ni kwamba siyo kweli jina "Yesu" kwa Kiarabu ni "Yasu" kama anavyodai wakristo. Ukweli ni kwamba Waarabu Wakristo jina "Yasu" ndilo jina walilolipokea kutoka kwa wale waliowapelekea ukristo ulianzishwa nje ya Uarabuni miaka mitatu baada ya Yesu au Nabii Issa (a.s) kuondoka. Na ndilo jina waliloliingiza ndani ya Injili ya Kiarabu. Na hii inafanana na jinsi baadhi hata ya Watanzania walivyopokea jina la yule Nabii Mbatizaji kwa matamshi tofauti. Baadhi yao walipokea kwa tamshi la "Yohana" (Kiyunani), wengine "John" (Kiingereza) na wengine "Yahya" (Kiarabu).

Ataonekana wa ajabu atakayedai leo kwamba tamshi mojawapo katika jina hilo hapo juu kwamba ni la Kitanzania (Kiswahili) eti kwa vile wanaolitumia jina hilo ni Watanzania na limeandikwa ndani ya Injili ya Kiswahili!

Pia Yesu kuitwa "mwokozi" hiyo siyo maana ya jina lake. Lakini "uwokozi" ni jina la kazi yake aliyopewa kuifanya (Mathayo 18:11). Hivyo, majina ya Yesu na Issa hayana maana yoyote zaidi ya kubaki kuwa ni majina tu. Na siyo lazima jina liwe na maana. Ila neno lenye maana ya "Wekundu uliozidiana na weupe" kwa Kiarabu (Baidawi Vol 1 Uk. 160) na siyo neno Issa.
(Matthew 18:11 does not appear in several current Bibles such as the New International Version, the New Century Version, the Contemporary English Version, Revised Standard Version and the New Living Translation... and is not found in the most reliable Greek manuscripts, such as the Siniatic and Vatican...)
Kwa mantiki hiyo, sababu hiyo (ya jina) bado haijamtofautisha Yesu na Issa. Lakini kama ilivyo kwa Yohana, Yahya au John, basi Issa na Yesu ni yule yule mmoja aliyezaliwa na Bikira Mariam (Qur’an 3:45 na Luka 1:26-31).

Isitoshe, Qur’an Tukufu ilipoeleza kwamba Nabii Issa siyo Mungu (5:72), hakusulubiwa (4:157-158), na ametumwa kwa wana wa Israeli peke yao (3:49), Waarabu waliokuwa Wakristo hapo kabla walimfahamu kwamba huyo ndiye "Yesu sahihi" aliyekana "Uungu" katika Biblia pia (Marko 12:29-34) na ndiye aliyenusuriwa kuuawa kama ilivyoelezwa na Qur’an Tukufu na Biblia pia (Waebrania 5:7) na kweli katumwa kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli peke yao (Mathayo 2:6 na 15:24).

Kilichofuatia baada ya kuelewa hivyo walisilimu na kumfuata Mtume Muhammad (s.a.w) ambaye ndiye Mtume pekee aliyetumwa ulimwengu mzima (Qur’an 21:107 na Yohana 16:7-14).
Pamoja na Waarabu hao, alisilimu pia aliyekuwa mfalme wa Ethiopia ya sasa (zamani Uhabeshi) Bw. Najash (Rejea historia ya maisha ya Nabii Muhammad (s.a.w.).


Hii hapa ni tafsiri ya jina "Yesu" katika lugha mbalimbali
Yesu ki Belarusian ni Ісус
Yesu ki Azarbaijani ni İsa 
Yesu ki Croatian ni Isus 
Yesu ki Indonesian ni Isa
Yesu ki Irish ni iosa
Yesu ki Italian ni Gesu 
Yesu ki Malay ni Isa
Yesu ki Persian ni Isa
Yesu ki Romanian ni Isus
Yesu ki Turkish ni Isa
Yesu ki Ukrainian Icyc
Yesu ki Urdu ni Isa
 


Utume 
Wakristo wanasema, ...Qur’an inasema Isa alipewa Injili ili kuja kuhakikisha yale yaliyokuwa kabla yake na kuisaidikisha Torati (Almaida 46). Biblia inasema Yesu alikuja hapa duniani kutafuta na kuokoa kilichopotea (Luka 19:10). Ndani ya Qur’an hakuna aya yoyote inayozungumzia kuwa Isa alikuja kuleta wokovu, je, hii si tofauti nayo? Mwisho wa kunukuu.
Wakristo waelewe kwamba siyo lazima Qur’an Tukufu itaje wazi kwamba Nabii Isa alikuja kuleta wokovu kama wakristo wanavyodai.
Kwa hali hiyo, hatuwezi kusema kwamba Bwana Yesu alikuja kuruhusu watu wamle nguruwe eti kwa vile hakusema wazi "msile nyama ya nguruwe", kama ilivyokatazwa na Mwenyezi Mungu (s.w.t.) katika Torati ya Musa.

Lakini ni dhahiri kuwa kule kusema kwake tu kwamba "msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua Torati wala Manabii, ila sikuja kutangua, bali kutimiliza" (Mathayo 5:17) kulitosha kuonyesha msisitizo na mkazo wa uharamu na unajisi wa kula nyama ya nguruwe kama ulivyotajwa wazi katika Torati (Kumbukumbu la Torati 14:8).

Kwa mantiki hiyo, kule kuja kwake (Yesu au Isa (a.s.) kuhakikisha yale yaliyokuwa kabla yake na kuisadikisha Torati kama Qur’an Tukufu inavyoeleza inatosha kukubali kwamba alikuja kuwaokoa waliopotea zama zake, ambao waliiweka kando miongozo sahihi ya Manabii wa kabla yake (Yesu au Isa) na Torati. Kwani inajulikana wazi kwamba Manabii na Torati waliokuwepo kabla ya Yesu au Nabii Isa hawakutumwa na Mwenyezi Mungu kuwatakia binadamu shari. Ila kuwatakia nusura (wokovu) mbele ya Mwenyezi Mungu siku ya mwisho (kiama) (Qur’an 2:213).

Na ndio maana Yesu akakana kuwatengua, yaani kuwapinga Manabii na Torati (Mathayo 5:17). Ni dhihiri alijua kazi na lengo la Mwenyezi Mungu kuwaleta (Luka 16:16-17).
Pamoja na ukweli huo, lakini wokovu mkubwa alioleta Nabii Isa au Yesu (a.s.) ni ule wa kuonyesha matokeo ya ushirikina, kama ule wa kumfanya na yeye kuwa ni Mungu pamoja na Mwenyezi Mungu (s.w.t.) aliyemtuma. Ambapo ni kinyume kabisa na mwenyewe alivyofundisha (tazama Marko 12:29). Alisema mtu huyo (anayemshirikisha Mwenyezi Mungu) Mwenyezi Mungu ameharamishia pepo na makazi yake ni motoni (5:72).

Kwa kweli huu hakika ndio wokovu mkubwa na wa kwanza aliouleta Nabii Isa. Kwani ni wazi kuwa maovu mengine yote chanzo chake kikuu ni shirki (kutomjua Mwenyezi Mungu vilivyo) (Ayubu 22:21).

Kwa mantiki hiyo, ni dhihiri kuwa Yesu na Isa ni yule yule mmoja aliyeleta wokovu kwa wana wa Israeli kama Qur’an na Biblia vinavyofundisha (Qur’an 3:49 na Mathayo 15:24).


Matendo yake
Katika kipengele hiki, wakristo wanasema... "Isa alipozaliwa tu alianza kuongea na kusema kuwa yeye ni mja wa Mwenyezi Mungu na amepewa kitabu na kufanywa Nabii (19:30-33). Biblia haielezi juu ya Yesu kutamka neno lolote siku ya kuzaliwa kwake." Mwisho wa kunukuu.

Ni kweli Biblia haikueleza lolote juu ya Yesu kuongea siku aliyozaliwa. Na haijulikani ni kwanini tukio zito na muhimu kama hilo lisigusiwe na Biblia! Hata hivyo, napenda kuwafahamisha kwamba si hilo tu liliachwa kuandikwa ndani ya Biblia lakini Bwana Yohana anatumbia kuwa:

"Kuna na mambo mengine mengi aliyoyafanya Yesu; ambayo yakiandikwa kwa moja kwa moja nadhani hata ulimwengu usingetosha kwa vile vitabu vitakavyoandikwa" (Yohana 21:25).

Kwa kauli hiyo ya Yohana inatosha kumwondoa wasiwasi mkristo yoyote iwapo atapata alililofanya Yesu au Isa (a.s) ndani ya Qur’an Tukufu ambalo halimo ndani ya Biblia Takatifu. Kwa kuwa litakuwa katika orodha ya mambo ambayo yalihofiwa kuandikwa moja kwa moja kama anavyotueleza Yohana ndani ya Biblia hapo juu. Kwa hali hiyo, hoja hiyo haiwezi kutofautisha Yesu na Isa.

Wakristo wanaendelea kusema... "Qur’an inasema Isa alitabiri habari za kuja Ahmad (Muhammad (61:6). Biblia inasema yeye ndiye "mwanzo na mwisho" hakuna mwingine tena (Ufunuo 21:6). Vile vile Yesu aliahidi kutuletea Roho Mtakatifu atakayedumu nasi milele (Yohana 14:14). Wala siyo Muhammad ambaye hakudumu milele. Mwisho wa kunukuu.

Kwa bahati mbaya wakristo katika kudai kwamba Bwana Yesu ndiye "Mwanzo na mwisho" amenukuu kitabu cha ufunuo wa Yohana. Hakujua kwamba mafundisho na miongozo ya kitabu hicho inawahusu Wayahudi peke yao. Na yeyote aliyejifanya kuwa ni Myahudi wakati siye, kitabu hicho kilimshutumu kwamba anatokana na kundi (sinagogi) la shetani. (Tazama Ufunuo 2:9).

Kwa hiyo, kitabu hicho kuwatoa wasiokuwa Wayahudi kunadhihirisha kuwa Bwana Yesu au Nabii Isa (a.s) ni "Mwanzo na mwisho" kwa Wayahudi. Ni wa "mwanzo" kwa Wayahudi kwa kuzaliwa bila ya baba (Luka 1:34-35) na ni wa "mwisho" kwa Wayahudi kwa kuwa baada ya yake haji tena Mtume mwingine kwa ajili ya nyumba ya Israeli tu. (Mathayo 21:33-34).

Kuhusu huyo Roho Mtakatifu aliyetabiriwa na Yesu bado ni Nabii Muhammad (s.a.w) kwa kuwa lipo sharti moja muhimu alilolitaja Bwana Yesu la kuondoka kwanza yeye (Yesu) ndipo huyo msaidizi mwingine aje. Na Mtume Muhammad (s.a.w) alitumwa na Mwenyezi Mungu.


Ukoo wa Yesu
Wakristo wanasema wananukuu... Qur’an inasema Mariamu aliyemzaa Isa ni binti Imrani (3:35 na 66:12). Ewe wa kizazi cha Harun, aliye kuwa Nabii Mchamngu Mahashumu!Vipi umefanya uliyo yafanya na baba yako hakuwa na tabia mbovu, wala mama yako hakuwa kahaba!

Maelezo ya Aya: ("Ewe dada wa Harun! Baba yako hakuwa mtu muovu, wala mama yako hakuwa kahaba." Imeandikwa katika Encyclopaedia Britannica kuwa Qur'ani imekosea kosa la kihistoria ilipo mwita Maryamu "Dada wa Harun," ilihali baina ya Maryamu huyu na Harun nduguye Musa ni karne nyingi. Wamesahau hawa kuwa Udugu ulio zungumziwa hapa ni wa kushabihiana. Makusudio ya hapa ni kushabihiana kwa wema na uchaMungu, yaani ewe uliye mshabihi Harun kwa wema na uchamngu, nini kilicho kugeuza hali yako njema ukawa hivyo?Wala baba yako hakuwa mtu muovu wa kutenda mabaya, wala mama yako kufanya uchafu. (Kadhaalika Maryamu ni ukoo wa Harun, na pengine huitwa "Binti wa Imran", na Imran ni baba yake Harun.)

Pia inaongeza kuwa Mariamu alikuwa dada ya Haruni (19:28). Biblia inasema dada ya Haruni ni Miriamu wala siyo Mariamu. (Kutoka 15:20). ... Biblia bado inaeleza kuwa Miriamu dada yake Haruni hajawahi kuzaa maisha yake yote. Mwisho wa kunukuu.

Ni kweli Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ndani ya Qur’an Tukufu amewanukuu Wayahudi kumuita Bi. Mariamu kuwa ni dada ya Harun. Pamoja na hivyo, "udada" unaokusudiwa hapo ni wa Kiukoo kwa kuwa Bi. Mariamu na Haruna wote wanatoka katika ukoo wa Lawi. Ushahidi wa hili tunaupata katika Injili ya Luka 1:36 inayoeleza uhusiano wa Mariamu na Elizabeti (mama yake Nabii Yohana Mbatizaji) ambaye ni mmojawapo wa uzao wa Haruni wa ukoo wa Lawi (Luka 1:5).

Kiutumishi wa kazi za Mungu, kwa kuwa Bi. Mariamu na Haruna wote walikuwa ni watumishi wa Mungu hasa kwa vile ukoo wao (Walawi) ndivyo Mungu alivyokwisha mteua maalum kwa kazi hiyo (Kutoka 40:12-16 na Luka 1:38).

Kiucha Mungu:
Kwa kuwa Bi. Mariamu alikuwa ni mcha Mungu neema aliyopewa na Mungu (Luka 1:30) kama vile Haruna pia. Na hii inafanana na ile kauli ya Bwana Yesu au Nabii Isa (a.s.) aliyosema:
"Kwa maana yeyote atakayefanya mapenzi ya Baba yangu aliye Mbinguni, huyu ndiye ndugu yangu, umbu langu na mama yangu". (Mathayo 12:50).

Hapa haina maana kwamba eti kwa vile Mkristo ataamua kufanya mapenzi ya Mungu basi ndio atakuwa ndugu ya Yesu wa kuzaliwa. Hapana! Lakini atakuwa ni ndugu yake kiimani (kiucha Mungu) tu.

Kwa mantiki hiyo, maelezo ya Qur’an Tukufu juu ya "udada" wa Mariamu kwa Nabii Haruna bado haujatofautisha Yesu na Isa. Lakini maana yake ni yule yule mmoja, Bikira Mariamu anayetajwa na Qur’an na Biblia kama tulivyoona hapo juu
.

Kuumbwa
Wakristo wanasema, ...Qur’an inasema Isa aliumbwa na Mwenyezi Mungu sawa na alivyoumbwa Adam (3:59). Hii ina maana kuwa Isa aliumbwa toka katika udongo. Biblia inasema Yesu alikuwako tangu milele yote kama nafsi ya Mungu (Yohana 17:5 na 1 Petro 1:20). Vile vile Biblia inasema alishuka toka mbinguni na kutwaa umbo la mwanadamu (Yohana 1:14). Yesu mwenyewe anasema yeye si wa ulimwengu huu bali ametoka kwa Baba (Yohana 8:23 na 16:28). Hii huoni kuwa ni tofauti?Mwisho wa kunukuu.

Qur’an kusema Nabii Isa au Yesu aliumbwa na Mwenyezi Mungu (s.w.t.) sawa na alivyoumbwa Nabii Adamu (a.s.):-

Mosi: Ni kuthibitisha (hakika) kwamba Bwana Yesu naye kama viumbe wengine aliumbwa na Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwani ni Mwenyezi Mungu pekee yake ndiye aliyeumba kila kitu (Isaya 44:24 na Qur’an 6:101-1020.

Pili: Yesu au Nabii Isa (a.s.) aliumbwa kwa tamko tu la Mwenyezi Mungu la kusema "kuwa na akawa" kama Adamu (a.s.) (3:59).

Tatu: Kwa kuwa Nabii Adamu (a.s.) (ndiye mtu wa kwanza kuumbwa) aliumbwa kwa udongo, vile vile Nabii Isa au Yesu (a.s) naye kwa kuwa alikaa tumboni mwa mama yake Bi. Mariamu kwa muda kadhaa ni wazi kuwa naye amerithi mwili ambao asili yake ni udongo kupitia mama yake. Hivyo, naye Yesu pia ni udongo kama Nabii Adamu (a.s.).

Biblia haijaeleza mahali popote kwamba Yesu ni nafsi ya Mungu kama wanavyo potosha wakristo wengi. Pia suala la kuwepo kabla ya ulimwengu si kwa Yesu peke yake bali ni kwa wanadamu wote (rejea Zaburi 90:1-2Waefeso 1:4 na Warumi 8:29-30) kwa shuhuda hizo, ni dhihiri kuwa binadamu wengine wote wana haki ya kusema "walitoka kwa Mungu", wakimaanisha kwamba "Muumbaji wao ni Mwenyezi Mungu".

Ama Bwana Yesu kusema kwamba yeye si wa ulimwengu huu haina maana nyingine yoyote zaidi ya kuonyesha ni jinsi gani asivyo thamini maisha ya kidunia na vishawishi vyake vyote badala ya maisha ya akhera. Na hii hata Mtume Muhammad (s.a.w) alikwisha ambiwa na Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwamba:
"…Na maisha ya dunia (hii) si kitu ila ni starehe idanganyayo (watu)"। (Qur’an 3:185).
Kwa hali hiyo, Yesu ndiye yule yule Nabii Isa bin Mariamu aliyeumbwa na Mwenyezi Mungu (s.w.t) bila ya baba kama Qur’an na Biblia vinavyoeleza.


Kuzaliwa
Wakristo wanasema ...Qur’an inasema Isa alizaliwa chini ya mtende tena wakati wa mchana (19:25). Qur’an haitaji mji aliozaliwa Isa. Biblia inasema Yesu alizaliwa katika mji wa Bathlehem wakati wa usiku katika zizi la ng’ombe (Luka 2:7). Je, huoni hiyo kuwa ni tofauti? Mwisho wa kunukuu.

Ni kweli Qur’an inaonyesha Nabii Isa alizaliwa chini ya mtende lakini hajaeleza kwamba siku hiyo ilikuwa ni mchana au usiku, pia Biblia haijaeleza kwamba Bwana Yesu alizaliwa katika zizi la ng’ombe kama wanavyozua wakristo.

Mstari huo wa Luka 2:7 wanao utaja wakristo (hapa juu) ulichoeleza ni kwamba baada ya Bi. Mariamu kumzaa Yesu alimlaza katika hori la kulia ng’ombe! Na hori siyo zizi la ng’ombe bali ni "mkondo wa bahari" (soma maelezo ya maneno katika Biblia, Uk. 1223, angalia herufi “H”). Hivyo, ni upotoshaji wa wazi wa maandiko kuzua kwamba Bwana Yesu alizaliwa katika zizi la ng’ombe!

Mara nyingi Qur’an Tukufu huzungumza msingi wa jambo tu kisha humwachia Mtume (s.a.w) atoe uchambuzi (Qur’an 16:44) kwa mantiki hiyo, Qur’an ilivyokwisha bainisha kwamba Nabii Isa au Yesu (a.s) amezaliwa na Bikira Mariamu, siyo lazima ieleze na mji aliozaliwa kwani siyo kitabu cha historia bali ni kitabu cha mwongozo na mazingatio kwa yote kinayoyaeleza n.k. (Qur’an 2:185 na 12:111).

Isipokuwa la kuzingatia hapa ni kuwa katika nchi ya Kiyahudi alikozaliwa Yesu au Nabii Isa (a.s) kama Qur’an Tukufu ilivyoeleza ni mashuhuri sana mitende (Yohana 12:12-13). Kwa hiyo, Qur’an kuonyesha kwamba Nabii Isa au Yesu alizaliwa chini ya mtende ilikuwa ni sahihi kabisa.

Na hii ni sawa na wanavyoamini Wakristo wenyewe kwamba Injili ya Yohana Mtakatifu kutoeleza kabisa historia ya kuzaliwa kwa Yesu bado hakujatofautisha na Yesu yule yule anayeelezewa na Injili ya Luka Mtakatifu iliyoeleza kwa kirefu historia ya kuzaliwa kwake (Issa (as) au Yesu)।

Na kama haitoshi, wakristo wanao ongea Lugha ya Kiajemi, Kikurdi, kituruki, Ki Irish n.k. Pia wanatumia jina la "Isa" sasa sijui hawa wakristo wanao tumia jina Issa badala ya Yesu, kwa mujibu wa imani ya wakristo wengine, je si wakristo kama wao? (Íosa – Issa au Jesu in Irish language)
.

1 comment:

  1. Mungu akuondoe kwenye upotovu hyo.Biblia haitafsiriwi kwa akili za kibinadam hvo.
    Mpotovu unaita wenzako wapotovu?
    Mungu akusaidie ujue kweli.

    ReplyDelete

Animated Social Gadget - Blogger And Wordpress Tips Twitter Bird Gadget