Thursday, April 26, 2012

Kwanini waislamu hamumwamini mtume Paulo?

Swali:
Kwanini waislamu hamumwamini mtume Paulo?


Jibu:
Hatumtambui Paul kwa sababu zifuatazo

1-Paulo ndo aloitengua torati:
Kumbuka Yesu alisema: "Msidhani ya kuwa nalikuja kutangua torati au manabii, sikuja kutangua, bali kutimiliza." Mathayo 5.17-20
Kazi yake haikuwa kutengua sharia ya Taurati na kuleta kitu kingine cha kutengua au kugonganisha na mafunzo ya sharia ya Mwenyezi Mungu na Mitume wake, bali kaja yeye kutimiliza kwa kuwafunza Mayahudi umuhimu wa mambo ya kiroho katika sharia. Kutii madhaahiri ya sharia tu na kuwacha undani wake, uchamngu, hakutoshi. Mwenyezi Mungu atiiwe kwa dhaahiri na kwa siri. Yesu alishikilia sana kufundisha na kutenda, aliposema: "Basi mtu ye yote atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndogo, na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni; bali atakayezitenda na kuzifundisha, huyo ataitwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni.


Katika amri za Taurati ni kama hii iliyomo katika Biblia:
Na nguruwe, kwa sababu yeye anazo kwato ni mwenye miguu iliyopasuka kati, lakini hacheui, yeye ni najisi kwenu. Msile nyama yao, wala msiiguse mizoga yao; hao ni najisi kwenu.(Mambo ya Walawi 11.7-8)
Kwa hiyo naliwaambia wana wa Israeli, Msile damu ya mnyama wa aina yo yote; kwa kuwa uhai wa wanyama wote ni katika hiyo damu yake; atakayeila awaye yote atakatiliwa mbali. Tena kila mtu atakeykula nyamafu, au nyama aliyeraruliwa na wanyama, kama ni mzalia, kama ni mgeni, atafua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hata jioni; ndipo atakapokuwa safi.(Walawi 17.14-15)

Hizo ni amri ziliomo katika Taurati, sharia ya Mungu, ambayo Yesu amesema kama ilivyo katika Injili ya Mathayo kuwa mwenye kuivunja ndogo yao na akawafundisha watu hivyo basi ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni. Na kuvunja hayo khasa ndio Paulo kafundisha. Msikieni:Kila kitu kiuzwacho sokoni kuleni, bila kuuliza-uliza, kwa ajili ya dhamiri; maana Dunia ni mali ya Bwana na vyote viijazavyo.(1 Wakorintho 10.25-26)

Mnamwona Paulo anavyobomoa sharia ya Taurati waliyoifwata Manabii wote, hata Yesu na wanafunzi wake thenashara, ya kuwa kuna vyakula vilivyo halali na kuna vingine ni najisi, haramu kuliwa, kama nguruwe, vya kunyongwa na damu? Yesu kafunza nini, na Paulo anafunza nini! 
Katika waraka wake aliowapelekea Wagalatia Paulo anasema:
Mmetengwa na Kristo, ninyi mtakao kuhesabiwa haki kwa sheria; mmeanguka na kutoka katika hali ya neema, Maana sisi kwa Roho tunalitazamia tumaini la haki kwa njia ya imani. Maana katika Kristo Yesu kutahiriwa hakufai neno, wala kutokutahiriwa, bali imani itendayo kazi kwa upendo.(Wagalatia 5.4-6)

Kwa kauli moja Paulo ameitengua sharia yote. Yesu kasema nini juu ya Mlima wa Zaituni na Paulo anasema nini katika barua yake kwa Wagalatia? Yesu alifuata sharia ya Mwenyezi Mungu na aliihishimu na akaahidi kuwa yeye hatoitengua kabisa, ila ataitimiza. Paulo anaibeza sharia na kuiona kuwa ni laana. Yesu akila kilicho halalishwa na Mungu, na alikiepuka kilicho harimishwa na Mungu. Paulo anatwambia tule kila kiuzwacho sokoni bila ya kujali dhamiri yetu. Yesu na Manabii wote tangu Nabii Ibrahim walitahiriwa kwa kufuata amri ya Mungu kama isemavyo Biblia:
Mungu akamwambia Ibrahimu, Nawe ulishike agano langu, wewe na uzao wako kwa vizazi vyao baada yako. Hili ndilo agano langu utakalolishika, kati ya mimi na wewe, na uzao wako baada yako, Kila mwanamume wa kwenu atatahiriwa.(Mwanzo 17.9-10)

2-Paulo mjuaji, anasema kumpinga Mungu:

Kwa sababu kutahiriwa si kitu, wala kutokutahiriwa, bali kiumbe kipya.(Wagalatia 6.15)
Katika barua yake aliyowapelekea Warumi ndio kabisa Paulo anaiangamiza sharia ya Mungu na kufanya vitendo kuwa havina maana yo yote.Chenye maana peke yake ni imani tu.

Basi, twaona ya kuwa wanadamu huhesabiwa haki kwa imani pasipo matendo ya sheria.(Warumi 3.28)
Kwa Paulo kuamini kuwa Yesu kafa msalabani na damu yake kuwa ni fidia kwa dhambi zetu ndio kwenye maana, sio kufuata sharia wala vitendo. Kwake yeye ile Taurati, ambayo Yesu mwenyewe hakuja kuitengua bali kaja makusudi kuitimiza, ni kifungo na pingamizi. Anawaambia Warumi:
Bali sasa tumefunguliwa katika torati, tumeifia hali ile iliyotupinga, ili sisi tupate kutumika katika hali mpya ya roho, si katika hali ya zamani, ya andiko.(Warumi 7.6)
Paulo anaiona Taurati ni kifungo, pingamizi, bali ni laana. Hayo sio maoni ya Yesu ambaye amesema: "Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaondoka." Je, kwa kuingia Paulo katika umoja wa Kikristo ndio tusema mbingu na nchi zimeondoka? Au kwa kutundikwa Yesu msalabani (ikiwa kweli katundikwa) ndio tuseme mbingu na nchi zimeondoka? Mbona watu wameyasahau upesi maneno ya Yesu mwenyewe, na kuyasikiliza ya Paulo? Kwa sababu yanakubaliana na matamanio yao? 

Mafunzo ya Paulo yalileta mzozano na ubishi mkubwa tangu pale mwanzo katika historia ya Kanisa baina ya kikundi chake cha Wakristo waliomfuata kutoka upagani, na wale Wakristo wa asli ya Kiyahudi. Wao walipinga moja kwa moja ile shauri ya kwenda kupelekewa mafunzo ya Ukristo mataifa waliokuwa hawakutahiriwa, wala hawaikubali sharia ya Taurati. Baadhi ya wanafunzi wa Yesu walikuwa hawakubali hata kula nao wale "wasiotahiriwa". Wao walikuwa wanajua vyema kuwa Yesu aliwakataza wasend kuwahubiria mataifa mengine isipokuwa Mayahudi tu, kwani ni wao ndio walikuwa wanaamini Mungu Mmoja na wao ndio wakiifuata sharia ya Mungu. Mwishoe ulifanywa mkutano na yakawapo baadhi ya masikilizano kuwa yafaa kuhubiriwa Ukristo kwa mataifa yasiokuwa ya Kiyahudu, na wao wasilazimishwe kubeba mizigo mizito katika dini kama vile wenye asli ya Kiyahudi. 

Walitumwa Paulo na Barnaba kuwaendea hao mataifa, nao ni Wazungu wa Kirumi na Kigiriki, na wakachukua barua iliomalizikia maneno haya muhimu:
Kwa maana ilimpendeza Roho Mtakatifu na sisi, tusiwatwike mzigo ila hayo yaliyo lazima, yaani, mjiepushe na vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, na nyama zilizosongolewa na uasherati. Mkijizuia na hayo mtafanya vema. Wasalamu.(Matendo 15.28-29)

Nyama zilizosongolewa, yaani nyama za kunyonga, zisiochinjwa. Yazingatieni haya si maamrisho ya Yesu, lakini ni masikilizano baina akina Paulo na wanafunzi wake Yesu,(kwa ridhaa ya Roho Mtakatifu) baada ya kuwa Yesu mwenyewe hayupo tena. Ikiwa hayo ndiyo waliokubaliana ilikuwaje Paulo tena kuwaandikia Wakorintho: "Kila kitu kiuzwacho sokoni kuleni bila ya kuuliza-uliza, kwa ajili ya dhamiri"? Lakini Paulo ni Paulo. 

Ndo maana namwamini Yesu Kristo/Mpakwa mafuta (amani ya Mungu iwe naye) na simwamini Paulo

No comments:

Post a Comment

Animated Social Gadget - Blogger And Wordpress Tips Twitter Bird Gadget